Home 2024 March 06 TUZIDI SANA KUTENDA KAZI YA BWANA

TUZIDI SANA KUTENDA KAZI YA BWANA

TUZIDI SANA KUTENDA KAZI YA BWANA

“Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana” (1 Wakorintho 15:58)

Tunapaswa kutambua kwa umakini kwamba, Mtume Paulo hapa anawasihi ndugu zake tu katika Kristo, wale ambao wamezaliwa mara ya pili kweli kweli – waliozaliwa katika familia ya Mungu.

Zaidi ya hayo, Mtume Paulo pia, alituma wito huu kwa Wakristo wote, kila mahali; kwa “wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu” (1 Wakorintho 1:2). Alijua kwamba kuna mwelekeo miongoni mwa waamini wote wa kushawishiwa kuacha kazi ya Bwana kupitia kuvunjika moyo au kutojali, hivyo anatusihi tuwe “imara” na “tusiotikishika,” huku akitukumbusha kwamba kazi yetu hiyo “siyo ya bure katika Bwana.”

Hakika, tunahitaji himizo hili! Kwa kawaida, hatuachagi biashara au nyumba zetu kwa kuzikatia tamaa kwa upesi. Tunataabika nazo licha ya shida na vikwazo mbalimbali, na wakati mwonekano unapokuwa mweusi au giza kuzidi zaidi sana, ndipo nasi tufanyapo kazi kwa bidii zaidi. Wakati mwingine, miili yetu huteseka kwa sababu hiyo, lakini hatukati tamaa asilani…!

Kuhusu kazi ya Bwana je, si zaidi sana? Roho nyingi za wale ambao Kristo aliokuja kuwafia zinaangamia katikati yetu na wala hilo halitunyimi usingizi. Ni wajibu wetu ulio wazi kuwaombea na kuwaambia juu ya upendo wa Mungu kwao. Na ni wajibu wetu pia kufanya kazi hii kwa bidii na kwa kujidhabihu ili ndugu hao wapate kuisikia na kuiamini habari njema ya wokovu wao. Je, tutajiteteaje siku ile, tutakaposimama mbele ya Mwokozi wetu; tukiwa mikono mitupu, bila ya kuleta hata roho moja iliyopotea kwake? Naye Je, atakuambiaje? (Mathayo 25:14-30).

Basi na tuwe na bidii katika kutenda hayo, “sikuzote tukiwa na wingi katika kazi ya Bwana.” Maisha haya ni mafupi sana na hatuwezi kupuuza nyakati hizi za thamani ambazo Mungu ametupa tuweze kutangaza neema yake ya wokovu. Hima, tusisite kuwaambia kwa vinywa vyetu na kwa maisha yetu pia kwa ushuhuda wetu na kwa tabia zetu, kwamba “Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi” na kwamba “tuna ukombozi kwa damu yake, masamaha ya dhambi kama vile wingi wa neema yake” (Waefeso 1:7).

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *