Home 2024 February 07 MATUMAINI MAWILI!

MATUMAINI MAWILI!

MATUMAINI MAWILI!

Ni ukweli usiopingika kwamba waumini wengi katika Kanisa leo hawajui wanakoelekea ‘watakapopita’ kutoka katika maisha haya ya kimwili; Kwamba wanauelekea Ufalme wa duniani, au wanaeleka kule juu mbinguni, au wataenda mbinguni kwa kitambo na kurejea tena katika nchi. Lakini unapoligawa Neno la kweli na kulitumia kwa halali (2 Timotheo 2:15), yote hayo yanawekwa wazi, na hivyo unaweza kujua kwa uhakika ni mahali gani unapoelekea.

Ufalme wa kidunia wa Kristo ni tumaini ambalo lilikuwa limetabiriwa na manabii wote wa kale na kuelezwa kwa uwazi katika Neno la Mungu (Yeremia 23:5-6; Luka 1:32-33):

“Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.”

“Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.”

Mada kuu ya unabii wote ni utawala wa Kristo duniani na kuinuliwa kwa Israeli pamoja Naye katika ufalme wake wa kidunia. Hili ndilo tumaini kwa taifa la Israeli kwa mujibu wa ahadi na maagano ambayo Mungu aliyafanya kwa taifa hilo. Kama Isaya 9:7 inavyosema kwamba “…Wivu wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo”, ni dhahiri kwamba hayo yote yatatimizwa!

Hata hivyo, Waisraeli walipomkataa Masihi wake (Matendo 2:22-24; 3:14-15) na kuendelea katika kutoamini kwao kwa kukataa huduma ya Mungu Roho Mtakatifu (Matendo 7:54-60), Mungu “alisimamisha” kwa muda mpango wake wa kinabii na Israeli na kuiweka kando katika kutokuamini (Warumi 11:11,15):

“Basi nasema, Je! Wamejikwaa hata waanguke kabisa? Hasha! Lakini kwa kosa lao wokovu umewafikilia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu.”

“Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa?”

Kisha Mungu, akaanzisha kipindi kipya, “kipindi cha neema ya Mungu” (Waefeso 3:1-12). Hivi ndivyo Kanisa, Mwili wa Kristo, ‘kiumbe’ ambacho hapo awali hakikuwepo (Waefeso 2:11-22), kilianzishwa.

Wakati wa kipindi hiki, wakati huu wa mabano wa urefu usiojulikana, sisi tunaoamini injili ya neema ya Mungu – kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, na kwamba alizikwa na kufufuka tena siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko (1 Wakorintho 15:1-4); tunakuwa washiriki wa Mwili wa Kristo na kuokolewa kutoka kwenye dhambi zetu kwa neema kwa njia ya imani pekee katika Kristo (Waefeso 2:8-9).

Sisi, kama washiriki wa Kanisa, Mwili wa Kristo, sio Israeli; Tumaini la Kanisa, Mwili wa Kristo, sio la kidunia. Tumaini letu si kutawala na kumiliki pamoja na Kristo duniani; bali ni kutawala na kumiliki pamoja na Kristo mbinguni (katika ulimwengu wa roho).

Tunaporejea nyaraka za mtume wetu, Mtume Paulo (Warumi 11:13), tunajifunza kuhusu mpango mpya wa Mungu; Mpango wa “siri,” ambao haukufunuliwa kabla ya kuitwa kwa Mtume Paulo (Wakolosai 1:24-27):

“Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake; ambalo nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu; siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu.”

Chini ya mpango huu mpya, Mungu amefunua tumaini jipya la kimbingu na wito kwa washiriki wa Kanisa, Mwili wa Kristo. Katika KWELI iliyofunuliwa kwa Mtume Paulo, tunajifunza juu ya utawala wa Kristo katika ulimwengu wa roho (Waefeso 1:20-23), na Mwili wa Kristo kuinuliwa pamoja Naye katika ufalme wake wa kimbingu huko juu sana mbinguni.

Katika Wakolosai 1:5, Mtume Paulo anarejelea “tumaini mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la kweli ya Injili.” Mtume Paulo hasemi tumaini ambalo limewekwa hapa duniani kwa ajili yetu katika Ufalme wa Milenia; badala yake, anasema kwamba kweli ya injili ya leo inatangaza tumaini lililowekwa kwa ajili yetu mbinguni (katika ulimwengu wa roho). Katika nyaraka zake, Mtume Paulo anafundisha juu ya Mwili wa Kristo kwamba:

Baraka zetu ni za kiroho na ziko mbinguni…

“Mungu … ametubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo.” (Waefeso 1:3)

Nafasi yetu iliyoinuliwa iko pamoja na Kristo mbinguni…

“[Mungu] akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.” (Waefeso 2:6)

Uraia wetu uko mbinguni…

“Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo.” (Wafilipi 3:20)

Hatutarejea duniani pamoja na Kristo wakati wa kuja kwake mara ya pili, atakapokuja kusimamisha ufalme wake wa kidunia; Hilo ndilo tumaini la taifa la Israeli. Tumaini letu la milele na makao yetu ya kudumu ni mbinguni na sisi, Mwili wa Kristo, tutatawala pamoja na Kristo milele katika ulimwengu wa roho…

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *