Home 2024 April 14 YEYE ALIYE WA KIROHO!

YEYE ALIYE WA KIROHO!

YEYE ALIYE WA KIROHO!

“Lakini mtu wa rohoni huyatambua [huyabaini] yote, wala yeye hatambuliwi na mtu” (1 Wakorintho 2:15).

Mtu ambaye ni wa kiroho kweli yuko juu sana kuliko wale wenye hekima zaidi wa ulimwengu huu; Naam, juu sana kuliko umati mwingi wa ‘Wakristo’ anaokutana nao, ambao yeye anaweza kuwaelewa, ingawa wenyewe ni vigumu (hawawezi) kamwe kumwelewa…

Hivyo, sote twapaswa kutamani kuwa wa kiroho ki-kweli kweli, ingawa swali litabaki kuwa; Je! Kuwa kiroho ki-kweli kweli, ni kuwaje?

Katika Nyaraka za Mtume Paulo, jamii ya wanadamu imegawanywa, kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, katika madaraja manne: Mtu wa asili; Mtoto mchanga katika Kristo; Mkristo wa kimwili; na Mkristo wa kiroho.

Madaraja haya yote manne (4) yanarejelewa katika kifungu kimoja cha Maandiko Matakatifu, yaani 1 Wakorintho 2:14 – 3:4, na ifahamike hapa kwamba madaraja hayo yameainishwa kulingana na uwezo wa wanadamu hao kufahamu na kuiga “mambo ya Mungu” kama yalivyofunuliwa katika Neno Lake. Kifungu husika kinasema hivi:

“Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu. Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo. Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu?”

Kupitia kujifunza Neno kwa bidii, na kwa maombi, na kwa hamu ya kweli ya kulitii, mtu wa kiroho atafikia kumjua Mungu na Bwana wetu Yesu Kristo kwa ukaribu zaidi na zaidi. Mtoto mchanga katika Kristo na muumini wa kimwili hawezi “kumtambua”, kwa sababu tu hamjui Mungu kama alivyo mtu wa kiroho. Lakini mtu huyo (mtoto mchanga na muumini wa kimwili), akiweza kukomaa kiroho, hakika ataweza kumwelewa Mungu na kumjua kabisa Bwana wetu Yesu Kristo; naye atakuwa ni miongoni mwa wale walioandikiwa haya:

“Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya” (Waebrania 5:14).

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *