Home 2024 April 04 DAUDI: MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU

DAUDI: MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU

DAUDI: MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU

Je! Umewahi kujiuliza, ni kwa jinsi Mungu alivyoweza kumwita Daudi kuwa ni “mtu aupendezaye moyo Wake” (1 Samweli 13:14)? Ni kweli kwamba, Mungu, alimwita hivyo Daudi, kabla ya yale makosa yake ya kutisha ya uzinzi na mauaji. Lakini, ni kweli zaidi kwamba, Mungu bado alimwita hivyo hivyo hata baada ya kifo chake: Mungu alisema haya, juu yake kwamba “alienda katika njia zangu, na kuyashika mausia yangu, na amri zangu” (1 Wafalme 3:14). Hili lakini, linawezekanaje?

Vyema, kwa kuanzia, linganisha jinsi Balaamu alivyoweza kusema juu ya Mungu kwamba “Yeye hakutazama uovu katika Yakobo, Wala hakuona ukaidi katika Israeli” (Hesabu 23:21). Hii, bila shaka, ilikuwa ndiyo sababu Wayahudi waliweza kusema kwamba “kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi” (Zaburi 103:12), na Isaya aliweza kuomba kwa uhakika akisema, “Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako” (Isaya 38:17). Kwa maana hiyo hiyo, Mungu aliweza kuzifumbia macho dhambi za Daudi, akijua kwamba siku moja Kristo angelipa kwa ajili ya dhambi hizo.

Hata hivyo, ni lazima kuwe na kitu cha zaidi kwa hilo ili Mungu aweze kumwita Daudi kuwa mtu anayeupendeza moyo Wake; Hata, wewe, naamini unaamini lipo! Je! Unaonaje, pale Mungu aliposema kuhusu Daudi kwamba moyo wake ulikuwa “mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake,”? Mungu, alisema hivyo kinyume na Sulemani, ambaye “wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine” (1 Wafalme 11:4). Ndiyo kusema, licha ya dhambi zake kuu, Daudi hakuanguka kamwe katika ibada ya sanamu. Daima, Daudi, alikuwa na moyo kwa ajili ya Bwana, na hamu kubwa ya kumtumikia Yeye peke yake.

Kama watumishi wa Mungu, mara nyingi waumini wanatuuliza jinsi tunavyoweza kuwafikiria wao kuwa ni ‘watu wema’, pamoja na makosa yao mengi yanayojulikana mbele ya macho yetu. Ikumbukwe, katika hali na namna nyingi, tumekuwa tukiwashauri waumini wetu, wanapopita katika nyakati za dhambi na kushindwa, na hivyo kibinadamu wengine wanakuwa na aibu ya dhambi zao ya ndani kabisa. Kimsingi, tunawaeleza tena na tena kwamba ni moyo wao kwa ajili ya Bwana ndio ambao Mungu hutazama.

Ndiyo kusema, wakati tunapaswa kujitahidi kila wakati, kuishi maisha yetu kwa ukamilifu kama vile Mungu anavyotuona katika Kristo (Wafilipi 3:10-14), na wakati huo huo bado wewe unajiumiza mwenyewe juu ya dhambi zinazokukumbusha kushindwa kwako hapo zamani; ni vyema ukafuta kabisa kumbukumbu hiyo akilini mwako na kuacha kabisa. Kumbuka kwamba “Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo” (1 Samweli 16:7), na kama Mungu hautazami uovu wako, wewe ni nani hasa unayepaswa kuutazama???

Hatimaye, ikiwa wewe ni mmoja wa muamini mwenye kuhukumu wengine katika makosa yao, ni kwa nini usijifunze kuwatazama wengine kama vile Mungu mwenyewe anavyokutazama wewe? Mungu mwenyewe ndiye aliyeagiza haya, akisema “mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe” (Warumi 15:7).

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *