Home 2024 February 06 HATARI YA KUJIVUNA!

HATARI YA KUJIVUNA!

HATARI YA KUJIVUNA!

Ujuvi kwamba Mungu ameweka migawanyiko katika Neno Lake, hakika, ni wa muhimu zaidi na ni wenye thamani sana. Inatusaidia kuelewa vyema kweli Yake katika Maandiko, na kutuwezesha kufuta kile ambacho kingeweza kuonekana kuwa ni ukinzani. Lakini pia kuna hatari mbili ambazo tunapaswa kuzifahamu na kuepukana nazo!

Mtego wa kwanza ni kuyatafuta tu “maarifa” tunaposoma Neno la Mungu. Ni vyema hapa usielewe vibaya kwa kile tunachojaribu kusema. Ujuzi wa fundisho la kweli (fundisho lenye uzima), au habari njema, kutoka kwa Neno la Mungu ni muhimu; tena ni muhimu sana. Mtume Paulo aliwaambia watakatifu wa Kanisa la Korintho alipowahudumia kwamba, “…nitawafaidia nini, isipokuwa nasema nanyi kwa njia ya ufunuo, au kwa njia ya elimu, au kwa njia ya hotuba, au kwa njia ya fundisho?” (1 Wakorintho 14:6). Mtume Paulo pia, hakuacha kuwatia moyo waumini kwamba “…wafanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha”, “walelewe katika…mafundisho mazuri” (1 Timotheo 4:6,13) na wawe wasitadi katika mafundisho yenye uzima (Tito 1:9; 2:1). Lakini, mtego ambao watu wengi hunaswa nao, ni kufikiri kwamba ni ‘maarifa’ pekee ndiyo tunayopaswa kuyatafuta pale tunapojifunza Neno la Mungu. Hili linapotokea, hutuacha tu na “majivuno” na “kiburi”. Kujifunza kwetu, kwa hiyo, kusituache pabaya zaidi katika kiburi cha maarifa na kutompendeza Bwana.

Mtego wa pili ni kushindwa kwetu kutafuta matumizi sahihi ya maarifa hayo katika kuyabadilisha maisha yetu ya kiroho. Paulo mtume aliwaambia watakatifu katika Warumi 6:17 kwamba, “Mungu na ashukuriwe, kwa maana mliitii kwa mioyo yenu ile namna ya elimu ambayo mliwekwa chini yake.” Mungu havutiwi na jinsi tunavyojua, isipokuwa tu hicho tunachokijua kinajionyesha katika maisha yaliyobadilishwa yenye utauwa mkuu. Kwa hivyo, kila wakati katika Maandiko, tunapaswa kuwa na uwezo wa kujibu swali hili kwamba: “Ni tofauti gani ambayo Mungu anataka habari hii ifanye katika maisha yangu leo?” Hiki ndicho ni kipengele muhimu zaidi cha kila somo la Biblia. Kwa hiyo, Jilazimishe wewe mwenyewe, na mwingine ye yote yule anayefundisha Neno la Mungu, kwamba matumizi ya aina hii ya maarifa ya Neno la Mungu yafanywe.

Hima, tusijivune kwa kiasi gani cha maarifa ya Neno la Mungu tunayoyajua, bali tugeuzwe kwa kuwa maisha yenye utauwa mkuu!

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *