Home 2022 May 29 Jedwali la Hadithi!

Jedwali la Hadithi!

Jedwali la Hadithi!

“… Kwa sababu hiyo uwakemee kwa ukali, ili wapate kuwa wazima katika imani; wasisikilize hadithi za Kiyahudi, wala maagizo ya watu wajiepushao na yaliyo kweli” (Tito 1:13-14).

Wale “wadanganyaji…”, “watu wa tohara” huko Krete (Tito 1:10) walikuwa wakizihubiri “hadithi za Kiyahudi” ambazo zilikuwa zikiwakengeusha na kuwageuza watu kutoka kwenye kweli ya Neno la Mungu, na kwa hiyo Paulo alimwagiza Tito awaambie watu wa huko wawaweke ndugu hao wa tohara kwenye orodha ya watu wasiotakiwa kusikilizwa…

Lakini hadithi hizi zilihusu nini hasa?

Kwa vyovyote vile zilivyokuwa, bila shaka, zilihusika na “amri za wanadamu” ambazo Paulo alisema zilikuwa pia zikitumika kuwageuza wengine (waamini) kutoka kwenye kweli. Na kwa kuwa hadithi hizo zilikuwa zikifundishwa (zikihubiriwa) na Wayahudi; wale watu wa tohara ambao walikuwa ‘hawajaokoka’, inaonekana ni jambo la busara kuamini kwamba zilihusu amri za wanadamu ambazo Paulo anawataja katika Wakolosai 2:21,22.

“Msishike, msionje, msiguse; amri… za wanadamu.”

Amri za wanadamu hapa zilikuwa ni amri za sheria ya Musa. Sheria hiyo ilijaa amri kuhusu vitu mbalimbali ambavyo havikutakiwa kuguswa, kuonjwa au kubebwa!

Unaweza ukawa unasema kuwa, “Lakini torati ilikuwa imebeba amri za Mungu, na wala si amri za wanadamu!” Na ungeweza kuwa uko sahihi – kama tungekuwa tupo chini ya sheria. Lakini mtume wetu, mtume wa neema, anasema “hatuko chini ya sheria, bali tupo chini ya neema” (Warumi 6:15). Na unapowaweka wanadamu chini ya amri zinazopatikana katika vipindi vilivyopita, amri hizo za Mungu hugeuka na kuwa ni amri za wanadamu. Ni jambo lenye umuhimu mkubwa sana, “kulitumia kwa usahihi/uhalali neno la kweli ya Mungu” (2 Timotheo 2:15)…!!!

Lakini kwa kuwa sasa tunajua ni amri zipi za wanadamu ambazo Paulo anamwonya Tito juu yake, hilo linatusaidia kujua asili ya hadithi hizo. Alikuwa akimuonya ajihadhari na watu wa tohara wanaofundisha sheria, na hatimaye kusimulia hadithi kuhusu sheria hiyo. Hadithi ni simulizi ambazo zilikuwa zinasimuliwa ili kufundisha somo fulani, na simulizi hizo ambazo Wayahudi hawa walikuwa wakizisimulia zilikusudiwa kufundisha somo kwamba tulikuwa bado tuko chini ya sheria.

Basi Je! Hizi zilikuwa ni hadithi za aina gani? Ni hadithi zile zile ambazo watu (hasa wale wanaojiita wa kiroho) wanazisimulia leo kuhusu sheria. Ni mara ngapi umesikia aya hii ikinukuliwa kutoka kwenye sheria?

Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako” (Kutoka 23:25).

Hiyo ilikuwa ni ahadi ya Mungu kwa watu wa Israeli wakiwa chini ya sheria. Lakini unapowaambia watu wanaonukuu mstari huo kwamba hatuko chini ya sheria, na hivyo hatuwezi kutarajia Mungu aheshimu ahadi hiyo, unasikiaga nini? Hadithi! “Lakini ndugu yangu Kufakunoga anamtumikia Bwana kwa uaminifu, na Mungu kwa sababu hiyo akamwondolea ugonjwa wake wa saratani ya koo!” Hiyo ni hekaya, hadithi iliyotengenezwa kufundisha somo kwamba bado tuko chini ya sheria…!!!

Sheria pia ilisema, “Mkumbuke BWANA, Mungu wako… maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri…” (Kumbukumbu 8:18). Hiyo pia ni ahadi nyingine ambayo Mungu aliwapa wana wa Israeli wakiwa chini ya sheria. Ikiwa tu “wangeisikiza sauti ya BWANA kwa bidii” (Kumbukumbu 28:1), Mungu aliahidi kuwazidisha mazao na mifugo yao (mstari wa 4,11,12).

Lakini unapowakumbusha watu leo ​​kwamba hatuko tena chini ya sheria ambapo ahadi hii inapatikana, unasikiaga nini? Hadithi juu ya hadithi! “Lakini Ndugu Oyoyo, kila mara amekuwa akimsikiliza Mungu, na sasa yeye amekuwa ni tajiri sana na anaweza kumudu kulipa ada zote za shule za Sekondari nchini!” Hadithi zisizokoma hizi zimetengenezwa ili kutufundisha somo kwamba bado tuko chini ya sheria ya Musa. Paulo anatuagiza tusizingatie hadithi kama hizo kamwe!

Kama nijuavyo kwamba unajua kuwa Wakristo wengi huweka hisa zao nyingi katika aina hizi za hadithi za mafanikio; hilo lisikushangaze, kwa maana Mtume Paulo alitabiri na kutuonya, akisema:

“Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.” (2 Timotheo 4:3-4).

Cha kusikitisha ni kwamba, unabii huu umetimia leo katikati yetu; ambapo Wakristo wengi wanapenda kuamini hadithi zinazosimuliwa kuliko kweli ya Neno la Mungu, lililogawanywa sawasawa.

Usiwe mmoja wao!

Ziainishe hekaya na ujiepushe nazo; rejea kwenye kweli ya neema ya Mungu kama iliyofundishwa na Mtume wako Paulo, na kamwe usiangalie nyuma tena – waache watu wa tohara waendelee na nasaba zao!

Utukufu una Yeye KRISTO, Milele na Milele; AMINA.

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *