Home 2020 August 22 Huduma ya Mauti Vs Huduma ya Roho

Huduma ya Mauti Vs Huduma ya Roho

Huduma ya Mauti Vs Huduma ya Roho

2 Wakorinto 3:6-18

“Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha. Basi, ikiwa huduma ya mauti, iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika; je! Huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu? Kwa maana ikiwa huduma ya adhabu ina utukufu, siuze huduma ya haki ina utukufu unaozidi. Maana hata ile iliyotukuzwa haikuwa na utukufu hivi, kwa sababu ya utukufu uzidio sana. Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu, zaidi sana ile ikaayo ina utukufu. Basi, kwa kuwa mna taraja la namna hii, twatumia ujasiri mwingi; nasi si kama Musa alivyotia utaji juu ya uso wake, ili kwamba Waisraeli wasitazame sana mwisho wa ile iliyokuwa ikibatilika; ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la Kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo; ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao. Lakini wakati wo wote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa. Basi <Bwana> ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru. Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho”

Paulo anasema kwamba sheria huleta lawama na kifo, wakati huduma ya Roho (Neema) inaleta uzima na uhuru. Sheria inadai haki kutoka kwa mtu mwenye dhambi lakini neema inatoa haki kwa mtu mwenye dhambi. Sheria inadai ukamilifu lakini neema inatoa ukamilifu

Sheria ilitolewa ili sisi tugundue kuwa tunahitaji mwokozi. Sheria hufanya kazi kama kioo na kuufunua udhaifu wetu wote na makosa yetu yote. Sheria haitoi haki kwa mtu yeyote yule bali sheria inamlaumu kila mtu. Kinyume chake, neema inaweza kumwokoa hata mmbaya zaidi kati yetu. Kwa dhabihu yake, Yesu ametukomboa kutoka kwenye sheria na hukumu yake.

Shetani bado anajaribu kutumia sheria kutukumu na kutupa hatia na aibu kila wakati tunapokosea. Hukumu hii inatutenga tusiwe na uhusiano wa karibu na Mungu. Sheria inafundisha kulipwa malipo tunayostahili. Neema ni juu ya upendeleo tusioustahili. Mungu hutubariki kwa sababu Yeye ni mwema, na wala sio kwa sababu ya wema wetu.

Neema inatuweka huru kutoka kwenye nguvu ya dhambi. Biblia inatufundisha kuwa nguvu ya dhambi iko kwenye sheria. Paulo alisema kuwa dhambi haitakuwa na nguvu juu yetu kwa sababu hatuko chini ya sheria bali tupo chini ya neema. Hatuwezi kujihukumia haki sisi wenyewe kwa jinsi ambavyo tumeishika sheria vizuri. Tukitambua kuwa Yesu ni chanzo chetu cha haki yetu, dhambi inapoteza nguvu yake na mashitaka yake kwetu.

Wakristo wengi wameshindwa na wamevunjika moyo (imani yao imekuwa dhaifu) kwa sababu wanaamini Mungu anawapenda tu pale wanapoishika sheria kikamilifu. Upendo wa Mungu kwetu hautokani na jinsi sisi tunavyofuata na kuishika sheria. Hasira zote za Mungu kwa ajili ya dhambi zetu zilimwangukia Yesu alipokuwa msalabani. Biblia iko wazi sana juu ya jambo hili kuhusu dhambi; Mungu ametusamehe dhambi zetu zote; ni jambo lililokamilishwa na wala sio ahadi!

Wakristo hawajakusudiwa kuishi maisha yenye hatia na aibu kwa sababu ya kushindwa kushika sheria. Kazi ya ‘Ukristo’ ilikamilika msalabani. Lazima tuache kujaribu kufanya kile ambacho tayari kimeshafanywa kupitia maisha yasiyokuwa na dhambi na dhabihu ya Yesu. Ukristo ni juu ya kupokea kile ambacho Yesu ameshakifanya tayari na sio juu kile ambacho sisi tunachokifanya.

Hukumu huua, neema inatoa uhai. Lazima tuache kuangalia mapungufu yetu na tuanze kuangalia kile Yesu alichokifanikisha pale msalabani. Kupitia Yeye hatuna lawama tena mbele za Mungu.

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *