Home 2020 March 17 Neema ya Mungu, Injili Iliyokataliwa!

Neema ya Mungu, Injili Iliyokataliwa!

Neema ya Mungu, Injili Iliyokataliwa!

Yesu Alilipasua Pazia, ‘Wakristo’ Wamelishona Upya!

Je, umewahi kuyasikia maneno ya Mtume Petro kuhusu ‘kongwa la Sheria ya Musa’ kwako na maonyo yake kwa wale wanaokubebesha? Anasema hivi: “Basi sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua” (Matendo 15:10). Na Paulo naye anasema hivi: “Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. Tazama mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno. Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote. Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema” (Wagalatia 5:1-4). Na Yakobo naye anasema hivi: “Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote” (Yakobo 2:10).

Pendo la Mungu ni kubwa sana kuliko vile unavyoweza kufikiri. Ukuu wake umepita akili ya kibinadamu inavyoweza kutambua, kama vile isivyoweza kuupima ukubwa wa ulimwengu ndivyo ambavyo ufahamu wa mwanadamu usivyoweza kulielezea pendo la Mungu lilivyo kwetu. Upendo wa Mungu hauna mipaka na wala hauwezi kuelezeka wala kufafanuliwa kwa akili za kibinadamu!

Neema ni jinsi Mungu anavyolidhihirisha pendo lake kwetu. Neema ya Mungu ni ya ajabu na haiwezi kuelezeka, na inatosha na inapita kila aina ya ‘ndoto’ mwanadamu anayoweza kuwaza kuiota. Na hiki ndo kitu pekee kinachoifanya imani ya Kikristo kuwa ya kipekee, ya namna yake; tofauti na imani zingine zote. Ukristo unatenganishwa na imani zingine zote duniani kwa sababu hiyo moja tu, NEEMA YA MUNGU; na wala sio kuacha dhambi, maombi, kutubu, au kuisha maisha ya utauwa, kwa sababu haya yote yanapatikana kwenye imani hizo zingine zote, kwa namna tofauti tofauti.

Neema ni upendeleo wa kipekee kutoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu Baba mwenyewe kwako kwa sababu ya upendo na wema wake. Neema ni kitendo cha Mungu kukuzawadia yeye mwenyewe (Yeye Mungu kujitoa mwenyewe kwako) bila sababu yo yote ile zaidi ya kwamba ilimpendeza yeye mwenyewe kufanya hivyo.

Je! Unahitaji ushahidi kudhibitisha hilo? Angalia msalabani ambako Kristo alikufa kwa sababu ya wasio na haki, wenye dhambi: “Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu” (Warumi 5:6) tena walipokuwa wangalipo katika kutenda dhambi zao: “Bali Mungu aonyesha pendo lake mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi” (Warumi 5:8).  Kristo kamwe hakufa kwa ajili ya wenye haki, watakatifu ambao hawakuwahi kumkosea Mungu, wale ambao walikuwa kileleni, watu wakuu, wasiokuwa na doa wakiwa juu ya ngazi. Kristo alikufa kwa ajili ya watu wanyonge na waliopotea na masikini na wahitaji.

Kristo aliutoa uhai wake kwa wale waliokuwa wakiuhitaji huo uhai. Kwa wale waaminifu vya kutosha ambao wanaweza kusema, “Nisaidie, Sina namna nyingine”, na Mungu anajibu kwa kusema, “Mimi ndio msaada wako mkuu.” Hiyo ndiyo neema! Neema sio fundisho (doctrine) bali ni Mtu na Jina lake ni Yesu. Neema sio moja ya baraka za Mungu bali ni jumla ya baraka zote zilizofungwa pamoja katika (ndani ya) Kristo. Neema ni Zawadi ya zawadi zote kutoka kwa Mtoaji wa watoaji wote. Neema, kama ilivyo kwa hewa ya ‘oxygen’, hatuwezi kuishi bila yenyewe na kwa hakika ye yote aliyeikosa hana uhai mbele za Mungu. Ni neema ya Mungu ndiyo iliyotuleta hapo tulipo na neema hiyo hiyo ndiyo itakayotufikisha kule tuendako.

Maandishi haya ni juhudi zangu za kumwambia kila mtu juu ya habari hii njema ya neema ya Mungu. Nakuandikia ili uweze kujua kwamba Mungu anakupenda vile ulivyo kwa kuwa ni Baba yako; haijalishi umefanya nini au umetenda mabaya kiasi gani, Baba yako wa mbinguni hakuhesabii hukumu kwa lolote lile. Anatamani akukumbatie na kukubusu na akutunze na kuwa na wewe milele yote.

Habari njema inayoleta furaha kuu ni kwamba Mungu hayuko kinyume chetu bali yupo kwa ajili yetu, yuko pamoja nasi, katika Kristo yupo ndani yetu. Je, liko jambo lolote unalodhani linaweza kututenga na upendo huo wa Mungu? Paulo anasema halipo, halijawahi kutokea; na kamwe halitokuwepo! “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho cho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Warumi 8:38-39). Unajua ni kwa nini? Ni kwa sababu hakuna jambo lililokuwa kubwa na ngumu kwa Mungu kama kumtoa (kumwua) mwanae pekee kipenzi aliyempenda kuliko vyote; lakini Mungu alifanya hivyo kwa ajiri yako! Ndio maana Paulo anakuuliza lipo jambo gani ngumu jingine lililobakia ambalo Mungu atashindwa kulifanya zaidi ya lile la kumtoa Yesu? Lipo? “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, ATAKOSAJE kutukirimia na mambo yote pamoja naye? (Warumi 8:32). Ukilijua hili ‘Ukristo’ utakuwa na maana kwako, wala hautahangaika kufanya au kujitahidi kuyatimiza yale ambayo Mungu alishayatimiza kwa ajili yako, kwa sababu yake yeye mwenyewe.

Neema ya Mungu, zaidi ya maelezo yo yote yale, ni bora zaidi kuliko ‘mkusanyiko’ wa dini zote za ulimwengu huu ukiziweka pamoja, ukiwemo na ‘Ukristo’. Dini zinasema ni lazima uwe ‘msafi’ (kwa viwango vyao) kabla hujaweza kumkaribia Mungu, lakini NEEMA inasema ‘njoo kama hivyo ulivyo!’ Kama ilivyo kwa mvuvi wa samaki, ambaye anamvua samaki na magamba yake, na uchafu wake wote, vile alivyo; na baada ya kumvua humtengeneza samaki huyo yeye mwenyewe kwa kadri anavyotaka kumtumia, pamoja na kumtia viungo; Mungu pia, ndivyo afanyavyo kwa sababu ya pendo lake.

Dini zinahitaji ufanye hili na lile ili ukubarike na Mungu, lakini neema ya Mungu inasisitiza Kristo Yesu alifanya yote, aliyakamilisha yote, wala hayahitaji nyongeza kutoka kwako! Dini zinasema ni lazima utunze sheria na kutoa dhabihu tena zinazouma, lakini neema ya Mungu inatangaza kuwa Kristo amezitunza na kuzitimiza sheria zote kwa niaba yetu na dhabihu aliyoitoa haina mbadala wake. Iko shida hapa, kwa sababu yale ambayo neema ya Mungu inayasisitiza yako kinyume na yale ambayo dini inayasisitiza; lakini OLE WAKE mtu yule anayeidharau neema ya Mungu:

“Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika NEEMA ya Kristo, na kuigeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe” (Wagalatia 1:6-8).

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *