Home 2021 November 19 Nimekuweka Kuwa Mlinzi!

Nimekuweka Kuwa Mlinzi!

Nimekuweka Kuwa Mlinzi!

Nabii Ezekieli aliteuliwa na Mungu kuwa “mlinzi” juu ya nyumba ya Israeli (Ezekieli 33:7):

“Basi wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu.”

Alikuwa na wajibu wa kuwaonya waovu waache njia zao mbaya, kwa kuwa ingawa Mungu alipaswa kushughulika na dhambi kwa haki, lakini Yeye mwenyewe alikuwa ametangaza hivi: “Sifurahii kufa kwake mtu mwovu; bali mtu mwovu aghairi, na kuiacha njia yake na kuishi” (Mstari wa 11):

“Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?”

Kama Ezekieli angeacha kuwaonya, waovu hao wangekufa katika dhambi zao, lakini damu yao ingedaiwa mkononi mwake. Lakini kama angewaonya kwa uaminifu, na wao wakakataa kutii onyo hilo; wangekufa katika dhambi zao, lakini damu yao isingedaiwa mikononi mwa Ezekieli (Mistari 8-9):

“Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.  Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako.”

Je, kuna Mkristo anayeweza kutukumbusha kwamba tunaishi chini ya kipindi kingine na kwamba ujumbe wetu ni wa neema? Huu ni ukweli usiopingika, na ukweli huo haupunguzi, bali unaongeza wajibu wetu kwa watu waliopotea.

Ikiwa sisi tulioamini, tunawaruhusu kwa uzembe wetu, watu waliopotea kwenda kwenye ‘makaburi yasiyo na Kristo’, Je! Hatuwajibiki ‘kiroho’ kwa maangamizi yao hayo?, na Je! Hatutawajibika katika Kiti cha Hukumu cha Kristo? Angalia kwa umakini mahusia haya ya Mtume Paulo katika 2 Wakorintho 5:10-11 juu ya jambo hilo:

“Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya. Basi tukiijua hofu ya Bwana, twawavuta wanadamu; lakini tumedhihirishwa mbele za Mungu. Nami natumaini ya kuwa tumedhihirishwa katika dhamiri zenu pia.”

Hii ndiyo sababu tunamwona Paulo akiwakumbusha wazee wa Efeso kwamba hakuwa ameacha kuwaonya watu “usiku na mchana, tena kwa machozi” (Matendo 20:31):

“Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi.”

Mtume Paulo alipogeuka nyuma na kutazama juu ya huduma yake kwa Waefeso aliweza kusema maneno haya: “Nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia” (Mstari wa 26-27):

“Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote. Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu.”

Na hii imekuwa ni kweli katika huduma yake yote kwa ujumla. Ama hakika, hii ilikuwa ni nia yake kwamba, kwa gharama yoyote ile, amalize mwendo wake kwa furaha, na huduma ambayo aliipokea kutoka kwa Bwana Yesu, ya kushuhudia “injili ya neema ya Mungu” (Mstari wa 24):

“Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.”

HIMA SOTE, tuendelee kumwomba Mungu, atupe sisi ambao ni waamini katika Bwana Yesu Kristo; MSUKUMO mkubwa zaidi wa kuwa na wajibu kwa wale waliopotea!!!

Kwa Utukufu Wake Yesu Kristo, AMINA.

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *