Home 2024 February 22 KUSIKIA NENO LA MUNGU DHIDI YA MENGINE…

KUSIKIA NENO LA MUNGU DHIDI YA MENGINE…

KUSIKIA NENO LA MUNGU DHIDI YA MENGINE…

Nafasi na umuhimu wa kusikia Neno la Mungu katika maisha ya mwamini, imeelezwa mara moja na kwa wakati wote na kwa watu wote, katika kumbukumbu iliyovuviwa ya ziara moja ya Bwana wetu Yesu Kristo katika nyumba ya wadada wawili, Mariamu na Martha:

“Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa” (Luka 10:38-42)

Ufafanuzi juu ya kifungu hiki kwa ujumla huonyesha kwamba wote wawili Mariamu na Martha walikuwa na mambo yao mazuri! Hili, bila shaka, ni kweli, lakini tukijiwekea kikomo kwa uchunguzi huu, tunaiba simulizi la somo lililokusudiwa, kwa kuwa Bwana wetu hakuwapongeza dada hawa wote wawili kwa “mazuri” yao. Alimkaripia Martha na kumpongeza na kumtetea Mariamu kuhusiana na jambo fulani mahususi.

Ni nini hasa, Mariamu alisifiwa kuwa nacho? Ni mara ngapi Mariamu ameonyeshwa kama mfano kwetu katika kutumia muda mwingi pamoja na Bwana katika maombi! Lakini hili, ni kukosa maana halisi ya kifungu husika! Mariamu hakuwa akiomba; bali alikuwa “ameketi miguuni pa Yesu, AKISIKILIZA NENO LAKE.” Aliketi tu pale, akinywa katika yote Bwana aliyotaka kuyasema…; Kwa kuwa hili ndilo agizo la Mungu mwenyewe:

“…Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye” (Mathayo 17:5)

Hilo lilikuwa ndilo “jambo moja la maana” ambalo Mariamu alikuwa ‘amelichagua’ na ambalo Bwana wetu alisema “halitaondolewa kutoka kwake”. Hivyo, ingawa sala na ushuhuda na matendo mema yote yana umuhimu wake katika maisha ya mwamini, lakini kusikia Neno la Mungu ndilo “jambo moja muhimu” juu ya mengine yote. Kwa hakika, hili “jambo moja muhimu” ni lazima lipewe mahali pake panapostahili na mengine yote yatafuata kikawaida.

Ni jambo linalokubaliwa, bila shaka, kwamba ni lazima tujifunze Neno la Mungu kwa maombi na kwa moyo mnyofu, vinginevyo litakuwa na matokeo mabaya, badala ya kutupatia matokeo yenye manufaa, na hili linaenda kuweka tu mkazo zaidi juu ya umuhimu mkuu wa Neno la Mungu, ambalo tunalitafuta; kwa kujifunza kwa dhati na kwa maombi, ili kulielewa na kulitii.

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *