Home 2023 December 11 YALIYOPUNGUA YA MATESO YA KRISTO!

YALIYOPUNGUA YA MATESO YA KRISTO!

YALIYOPUNGUA YA MATESO YA KRISTO!

Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake” (Wakolosai 1:24)

ANGALIZO:

Ipo tofauti katika ya:

Yale yaliyopungua “YA” mateso ya Kristo; na

Yale yaliyopungua “KATIKA” mateso ya Kristo; kama LUGHA ina maana!

Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu – Kwa ajili yenu kama sehemu ya ulimwengu wa watu wa Mataifa. Mateso yake hayakuwa kwa ajili ya Wakolosai peke yake, bali Mtume Paulo alijiona kuwa anateseka kwa sababu ya kazi yake ya kuwahubiria injili wapagani (watu Mataifa) kwa ujumla wake. Majaribu yake kule Rumi (na mahala pengine kabla ya Rumi) yalikuwa yamemfika kwa sababu alikuwa amesimamia kutangaza kwamba ukuta wa farakano kati ya Wayahudi na Mataifa ulikuwa umebomolewa (Waefeso 2:11-22), na kwamba injili ilipaswa sasa kuhubiriwa bila ubaguzi kwa wanadamu wote.

Tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo – Yale ambayo siwezi kuyafikia; mateso ambayo Kristo aliyastahimili kwa ajili ya kanisa! Katika hili, Mtume Paulo anaonekana kumaanisha kwamba alikuwa bado hajateseka vyakutosha kama vile (kumfikia) Kristo alivyoteseka na ingawa alikuwa ameteseka sana! Kulikuwa na mengi ambayo yalikosekana (yalipungua) ili kumfanya awe ‘sawa’ na Kristo Mwokozi katika jambo hilo; Kama kungekuwa na uwezekano huo…

Anachosema hapa kinatokana na tamanio kuu la roho yake – kanuni kuu ya maisha yake – kuwa sawa na Kristo; sawasawa katika tabia ya kimaadili, katika mateso, na katika hatima (Wafilipi 3:10). Akiwa na shauku hii kubwa, alikuwa ameongozwa kufuata njia ya maisha ambayo ilimpeleka katika majaribu yanayofanana sana na yale ambayo Kristo mwenyewe aliyavumilia; na, kwa haraka iwezekanavyo, alikuwa akiyapitia (akiyajaza) yale ambayo yalikuwa yamekosekana (kwake yeye).

Ifahamike hapa kuwa, Mtume Paulo hamaanishi kwamba kulikuwa na kitu chochote kilichopungua au kulikuwa na upungufu katika mateso ambayo Kristo aliyastahimili katika kufanya kwake upatanisho ambayo yalipaswa kuongezwa (kusaidiwa) na wafuasi wake, ili matokeo mema ya kazi zao hao, yaongezwe kwake (Kristo) ili aweze kuwapatia wanadamu wokovu kamili, kama baadhi ya watu wanaonekana kudhani; bali kwamba, bado kulikuwa na upungufu mwingi kwa upande wake kabla hajafananishwa kabisa na Mwokozi wetu, katika mateso yake.

Tafsiri ya kawaida ni, “yale yaliyosalia kwangu katika kustahimili dhiki kwa ajili ya Kristo.” Lakini hili linaonekana kuwa limepoa, na wala haliwezi kukidhi fikra za Mtume Paulo!!!

“Ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu” (Wafilipi 3:10-11)

Utukufu Una Yeye Kristo Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *