Home 2023 December 07 HEKIMA YA SULEMANI NA HEKIMA YA PAULO!

HEKIMA YA SULEMANI NA HEKIMA YA PAULO!

HEKIMA YA SULEMANI NA HEKIMA YA PAULO!

1 Wafalme 3:11-13 & 1 Wakorintho 3:10-11

Hekima ya Sulemani na hekima ya Paulo LAZIMA zitafsiriwa ndani ya muktadha wa Agano walilokuwemo; mmoja la KALE na mmoja JIPYA, ili kuweza kulitendea HAKI, AGIZO lililomo katika 2 Timotheo 2:15! Kwa hiyo, hekima ya Sulemani zilikuwa ni ya “KIMWILI” kama lilivyokuwa AGANO alilokuwemo na hekima ya Paulo zilikuwa ni ya “KIROHO” kama ilivyokuwa AGANO alilokuwemo. Kimsingi, “hekima” zao zilikuwa ni ‘uwezesho’ wa kiungu, ndani ya Agano husika ili waweze kuyatenda yanayowastahili, sawasawa na kusudi la umilele la Mungu. Ukisoma mafungu hayo mawili, tofauti hii, ni dhahiri kabisa:

“Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu;  basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe.  Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.”

“Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake.  Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo.”

 

HEKIMA YA SULEMANI

“Moyo wenye busara na uelewevu” – hekima ya Sulemani, inaonekana kuwa ya maadili na ya kiakili:

“Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani. Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri. Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka. Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano. Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.  Wakaja wa mataifa yote ili waisikie hekima ya Sulemani, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake.” (1 Wafalme 4:29-34).

Ndio kusema, ilikuwa ni hekima ya maadili peke yake ambayo aliomba, na ambayo aliahidiwa. Maneno yaliyotafsiriwa “busara” na “ufahamu,” yote yanaashiria hekima inayotumika. (Tazama Mwanzo 41:33, Mwanzo 41:39; Kumbukumbu la Torati 4:6; Mithali 1:2, n.k.)

“Wala baada yako hakutatokea mtu kama wewe”  i. e. katika ufahamu wa kile kilichokuwa ndani ya mwanadamu, na katika hekima ya kuongoza mwenendo wa mwanadamu, alikuwa awe mwenye busara zaidi ya “watu wengine wote” (wa kawaida). Katika hekima kama hiyo ulimwengu ungemjua mmoja tu “mkubwa kuliko Sulemani” – Mathayo 12:42; Luka 11:31.

Je! Mitume hawakumshinda?

Hawakufanya hivyo kwa maarifa ya asili na ya kisiasa, bali tu kwa maarifa ya siri za imani, ambazo zilitolewa kwa uhuru na kwa ukamilifu zaidi nyakati zao; ujinga wa wakati huo, haukuwa na dharau kwa hekima ya Sulemani, kwa sababu haukuweza kugunduliwa na kiumbe chochote bila ufunuo wa Kimungu, ambao Mungu aliona haungefaa kuhimidiwa wakati wa Sulemani. Hatuna haja  ya kutumia nguvu yoyote katika kudhibitisha kwamba uwezo wa asili wa Sulemani ulikuwa juu kuliko mitume wote; na Sulemani alikuwa na maarifa kamili ya vitu vyote vilivyojulikana katika enzi hiyo, kuliko mitume walivyokuwa katika ‘uvumbuzi’ wote wa umri wao.

 

HEKIMA YA PAULO

Kwa kadiri ya neema ya Mungu” – Hili Paulo analisisitiza, ili asije akaonekana kujipa mwenyewe kitu chochote (utukufu); “kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima” – mbunifu hodari, aliyeongozwa na hekima ya kimungu; “Naliuweka msingi” – ambao ni Yesu Kristo naye amesulibiwa, msingi  unaotosha kubeba ‘nyumba yote’ ya Ukristo, na matokeo yake yote yenye baraka: “na mtu mwingine hujenga juu yake” – Walimu wanaofuatia hufanya kazi zaidi katika mafundisho ya msingi na yenye kuwajenga wanafunzi. “Lakini kila mtu – kila mhudumu; na angalia jinsi anavyojenga juu yake” – Ili mafundisho yote anayofundisha yawe yanalingana na msingi uliowekwa. “Maana msingi mwingine” – ambao kanisa lote, pamoja na mafundisho yake yote, upendeleo, na majukumu, yanaweza kujengwa; “hakuna mtu awezaye kuuweka” – Hata kama atajaribu kufanya hivyo kwa kiasi gani; “isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa” – Katika mashauri ya hekima ya kimungu, katika unabii na ahadi za Agano la Kale, na katika mahubiri ya Kristo mwenyewe na mitume wake, hususani Mtume Paulo; “yaani, Yesu Kristo” – Ambaye katika nafsi yake na huduma zake, katika upendo na mateso yake, aibu yake na kuinuliwa kwake, kifo chake cha upatanisho, ufufuko wake wa ushindi, kupaa kwake kwa utukufu, na maombezi yake yasiyokoma, ndiye mwamba thabiti, usioweza kuyumba hata milele; msingi mtoshelevu hubeba uzito wote ambao mwenye dhambi, anapoamini, anaweza kuweka juu yake, hata kuwa na matumaini ya kutokufa. Kristo, katika ofisi yake ya unabii, kama mwalimu atokaye kwa Mungu, ndiye msingi wa mafundisho yote ya Ukristo, na kama yalivyofanywa na Mungu kuwa hekima kwetu, chanzo cha maarifa yetu, na imani katika mafundisho hayo. Katika ofisi yake ya ukuhani, hutupatanisha na kutuombea, ndiye msingi wa ‘marupurupu’ (thawabu) yote ya Ukristo; na, alipofanywa na Mungu kuwa haki yetu, ametuweka sisi waamini katika miliki ya hizo haki; katika ofisi yake ya kifalme yeye ndiye msingi wa majukumu yote ya Ukristo, na Mungu alipomfanya kuwa utakaso wetu, alitupa nguvu/uweza wa kutekeleza majukumu hayo; kwani mti ukiwa ni mzuri, matunda yake huwa mazuri pia; tunapoumbwa upya katika Kristo Yesu, matendo mema ni matokeo yasiyoepukika kamwe (Waefeso 2:10).

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *