Home 2023 May 01 HUNA UDHURU!

HUNA UDHURU!

HUNA UDHURU!

Sura ya Pili ya Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi ni kifungu chenye ‘giza’, ni kifungu chenye kusikitisha, lakini kifungu hicho kinafungua mlango wa baraka nyingi sana ambazo moyo wa mwanadamu unaweza kuwa nazo: WOKOVU KWA NEEMA.

Maneno ya utangulizi: “Kwa hiyo huna udhuru,” yapo wazi kweli kweli, lakini Mungu hufichua hali yetu ya dhambi ili tu aweze kutuokoa nayo.

Hapa ndipo falsafa nyingi zinapogongana ana kwa ana na Biblia! Falsafa hizo hufunga ‘macho yake’ kwa asili ya dhambi ya mwanadamu. Wanabishana, kwa ujumla, kwamba mwanadamu kwa asili ni mwema, wakati ushahidi mwingi unashuhudia kwamba yeye ni mbaya. Kwa hiyo, falsafa hizo za kibinadamu hazitoi ‘wokovu’ dhidi ya dhambi na adhabu yake ya haki. Ni Biblia pekee inayofanya hivyo kwa “injili [yake ya habari njema] ya neema ya Mungu.”

Katika nyakati za Mtume Paulo, wanafalsafa Wakiyunani waliwashutumu wapagani wasiostaarabika kwa uasherati na uovu wao wa waziwazi. Lakini katika kuhubiri kwao wema huo, waadilifu hawa, nao wenyewe walitenda maovu, na Mungu akasema:

“Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, HUNA UDHURU; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale” (Warumi 2:1).

Ni vivyo hivyo leo pia. Umati wa watu wa kutosha, wanajiona kuwa ni watu waadilifu na wenye tamaduni na maadili (kwa nje), lakini wanasahau kwamba Mungu anaangalia moyo na anaiona chuki kama mauaji; wivu kama wizi na sura ya ashiki kama uzinzi. Mungu hakiangalii kile tunachofanya, kwa nje, bali kile tunachotamani kufanya au kile tunachotaka kuthubutu kufanya. Anaona matamanio na nia za moyo!

Lakini ashukuriwe Mungu, “Kristo alikufa kwa ajili ya wenye dhambi” – wenye dhambi na wenye hatia, na wote wanaokuja kwa Mungu kwa imani katika Kristo “wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu” (Warumi 3:24).

Je! Ni “Huna udhuru,” au “Unahesabiwa haki bure kwa neema Yake,” kupitia imani katika Kristo aliyekufa kwa ajili ya dhambi zetu?

UTUKUFU NA UWEZA NA UKUU VINA YEYE HATA MILELE AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *