Home 2023 April 28 Ushauri wa Mama Maria!

Ushauri wa Mama Maria!

Ushauri wa Mama Maria!

“Lo lote atakalowaambia, fanyeni” (Yohana 2:5)

Wakati ule, kwenye karamu ya arusi ya Kana ya Galilaya, mamaye Yesu alipoona divai imewatindikia, kwa mara ya kwanza, alimwendea mwanawe ili kupata msaada, lakini mama huyu ‘alipokea’ jibu ambalo wanatheolojia wote kwa karne zote hawajaweza ‘kulilainisha’: “Mwanamke, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia” (Yohana 2:4).

Mama Maria alitakiwa ajifunze somo gumu, lenye uchungu, kwamba Yesu kama Mwana wa Mungu ni lazima akanushe madai ya ye yote yule ambaye angejivunia uhusiano wa karibu Naye kwa misingi ya kuzaliwa kimwili.

Mama Maria alipaswa asimfikirie Yesu kama “Mwanangu”. Kama ilivyo kwa mwanadamu mwingine ye yote yule, alitakiwa ajifunze kumjua Yesu kama Bwana na Mwokozi Wake.

Hata hivyo, mwamini mnyenyekevu Mama Maria, aliweza ‘kulichukua’ somo hilo gumu vizuri. Kabla ya hili, pale Yesu alipokuwa amezungumza kwa mtindo kama huo, mamaye huyu “aliyaweka hayo yote moyoni mwake” (Luka 2:51). Kisha Mama Maria akaenda kwa watumishi wake na kuwaambia: “Lo lote atakalowaambia, fanyeni”.

Maria, mama mpole na mnyenyekevu, angefanya vivyo hivyo leo kwa ye yote yule. Kama angeweza kupata fursa ya kusema hadharani leo, angewaelekeza waabudu wake kwa Bwana Yesu Kristo, na kusema: “Lo lote atakalowaambia, fanyeni”.

Ajabu ni kwamba, waumini wengi wanaonekana kufikiri kwamba maneno ya Yesu Kristo ni yale tu ambayo Alizungumza alipokuwa hapa duniani. Wamesahau au hawajajua kamwe kwamba Bwana wetu Yesu Kristo alisema tena kutoka mbinguni kwa ufunuo kwa Mtume Paulo na kwamba katika nyaraka zake tunayo maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo kwetu leo ​​(angalia Wagalatia 1:11-12; 2:7-9):

“Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo”

“Bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa; (maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa Mataifa); tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara”

Mtume Paulo alikuwa, kwa maana ya pekee, balozi/mjumbe wa Bwana aliyekataliwa. Kwake ilikabidhiwa “injili ya neema ya Mungu” (Matendo 20:24) na siri ya “kusudi la milele” la Mungu (Waefeso 3:1-11). Katika kumalizia Waraka wake wa kwanza kwa Timotheo, aliandika hivi:

“Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali MANENO YENYE UZIMA YA BWANA WETU YESU KRISTO, wala mafundisho yapatanayo na utauwa, amejivuna; wala hafahamu neno lo lote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo hutoka husuda, na ugomvi, na matukano, na shuku mbaya;  na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida.” (1 Timotheo 6:3-5).

Vivyo hivyo, kwa Wakorintho wasiotii aliandika:

“Nimetangulia kuwaambia; na, kama vile nilipokuwapo mara ya pili, vivyo hivyo sasa nisipokuwapo, nawaambia wazi wao waliotenda dhambi tangu hapo, na wengine wote, ya kwamba, nikija, sitahurumia; KWA KUWA MNATAFUTA DALILI YA KRISTO, ASEMAYE NDANI YANGU, ambaye si dhaifu kwenu, bali ana uweza ndani yenu” (2 Wakorintho 13:2-3)

Ushauri wa Mama Maria leo ​​ungekuwa ni kuamini injili ambayo Mtume Paulo alihubiri, “Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa KRISTO ALIKUFA KWA AJILI YA DHAMBI ZETU, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko” (1 Wakorintho 15:3-4).

UTUKUFU UNA YEYE MUNGU KWA KRISTO YESU AMINA

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *