Home 2022 December 16 MAADUI WA MSALABA!

MAADUI WA MSALABA!

MAADUI WA MSALABA!

“Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni ADUI ZA MSALABA WA KRISTO; mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani.” (Wafilipi 3:18-19)

Wakati wa ziara za kitume za Mtume Paulo huko Ulaya ya kipindi chake, alikuwa akiwaonya mara kwa mara Wafilipi kuhusu watu ambao hawakuwa kitu chochote zaidi ya kuwa tu ni watu wadanganyifu. Ni wazi kwamba tatizo la watu wadanganyifu katika makusanyiko hayo lilikuwa limeongezeka sana wakati ule mpaka kumfanya Mtume Paulo aandika maneno haya; “Nimewaambia habari zao mara nyingi, na sasa nawaambia hata kwa machozi.”

Watu hawa walikuwa wametiwa alama na Mtume Paulo kama “adui za Msalaba wa Kristo.” Huenda, ndugu hao, walikuwa wakionekana kwa nje kuwa kama watu wa DINI (watauwa) lakini kimsingi walikuwa hawamchi Mungu, bali walikuwa wakizisukuma agenda zao binafsi; walikuwa ni watu wenye viburi, watu wenye tabia za kimwili na watu wasiokuwa na imani.

Kuna mashitaka makuu matatu ambayo Mtume Paulo ameyatoa dhidi ya watenda maovu hawa:

Kwanza, kwa kufuata mpangilio wa uwasilishaji katika kifungu hicho, ni kauli kwamba; “ambao mwisho wao ni uharibifu.” Hakika hii, haiwezi kusemwa juu ya wale wote waliookolewa katika uhalisia wake; Lakini Kwa upande mwingine, ni jambo lililo dhahiri kwamba, kwa wale wote ambao hawajaokolewa watapata uharibifu wa milele kama ilivyotabiriwa katika 2 Wathesalonike 1:7-9 bila kujali walipo.

Pili, ni lile lengo la ibada yao. Je! Walikuwa wakimwabudu Mungu wa kweli na aliye hai? Hapana! mungu wao alikuwa ni tumbo lao – tamaa za kimwili, ambazo zilileteleza tamaa zisizotoshelezwa katika jitihada zao za kutosheleza hamu za miili yao.

Tatu, tunaambiwa waliweka mapenzi yao kwenye mambo ya kidunia pekee kama vile: falsafa, akili, nguvu, umaarufu, bahati n.k.

Ndio maana Mtume Paulo anawaita watu hawa kuwa ni maadui wa Msalaba, kwa sababu “walikuwa ni wenye mfano wa utauwa, lakini wakizikana nguvu za Mungu.” Wajumbe hawa wa Shetani hawakuwa na hamu ya kuelewa mahubiri ya Msalaba, ambayo kwayo wangeweza kuhesabiwa haki katika mambo yote.

Mambo hayajabadilika sana, leo walaghai hawa kwa ujasiri, wameubadilisha ujumbe wa injili na kuwa mafundisho ya ‘fikira chanya’, ambayo ‘yamewaongoza’ wengi kwenye hisia zisizo za kweli za usalama katika kufikiri kwamba wako sawa na Mungu. Inasikitisha kusema hapa kwamba, hata baadhi ya waamini waaminifu, ‘wameangukia’ chini ya ‘uchawi’ wa mafundisho haya ya hila.

Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba, ingawa MSALABA wakati fulani unazuiliwa na kupigwa vita, lakini bado unaendelea kuwa “nguvu ya Mungu iletayo wokovu.”

Jihadharini sana na maadui hao wa Msalaba, wako katikati yetu leo hii; tena ni wengi, wala si wachache!

UTUKUFU UNA YEYE MILELE NA MILELE AMINA

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *