Home 2022 November 04 Mambo Mawili Tuyajuayo!

Mambo Mawili Tuyajuayo!

Mambo Mawili Tuyajuayo!

Katika Warumi 8 Mtume Paulo anatuelekeza kwenye KWELI kuu mbili ambazo kila mwamini wa kweli anatakiwa kuzijua. Kweli ya kwanza ipo katika mistari ya 22-23, ambapo ujuvi unapatikana kwa uzoefu; na kweli ya pili ipo katika mstari wa 28 ambapo ujuvi unapatikana kwa imani.

Katika Warumi 8:22-23, Mtume Paulo ametuandikia hivi:

“Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa. Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu.”

Maneno “hata sasa,” katika kifungu hiki, ni ya maana sana, kwa kuwa Bwana wetu alikuja duniani akiwaponya wagonjwa, akiwasafisha wenye ukoma, akiwafanya vipofu waone, viziwi wasikie na vilema waruke-ruke kwa furaha. Lakini, pamoja na yote hayo, alikataliwa na watu wenye dhambi na kupigiliwa misumari msalabani.

Baada ya ufufuko wake na kupaa kwake mbinguni, watesi wake hao walipewa nafasi nyingine; kupitia wito wa Mtume Petro, ambaye aliwaita watubu ili “zipate kuja nyakati za kuburudishwa” ambazo zitatokana na “kuwako kwake Bwana” (Matendo 3:19,20). Lakini, pamoja na yote hayo pia, Mfalme alikataliwa na ufalme Wake uliobarikiwa ulikataliwa ili kwamba, kwa maneno ya Paulo, uumbaji wote uendelee kuugua na kuwa na uchungu “pamoja hata sasa.”

Lakini katika kifungu hiki Mtume Paulo anaonyesha kwamba hata watoto wa Mungu hawajaachiliwa kutoka katika mateso haya, kwa maana mwamini mwaminifu zaidi, mtakatifu aliyewekwa wakfu zaidi, bado anapaswa kushiriki katika mateso na huzuni za ulimwengu wakati akingojea “ukombozi wetu wa mwili,” wakati ambapo “sisi sote tutabadilishwa” (1 Wakorintho 15:51).

Lakini ingawa kila mwamini anajua kuhusu mateso haya na huzuni kwa uzoefu, kuna kitu kingine ambacho mwamini huyo anakijua kwa imani. Mstari wa 28 unazungumza juu ya hili:

“Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”

Mkristo wa kweli si mtu mwenye kujawa na matumaini tu; bali yeye ni mtu anayeliamini Neno la Mungu, na Mungu ana mengi ya kusema kuhusu jinsi Anavyofanya kazi yote kwa manufaa Yake mwenyewe. Tunayo nafasi hapa ya kunukuu angalau vifungu viwili:

“Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi.” (2 Wakorintho 4:17)

“Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu utakaofunuliwa ndani yetu.” (Warumi 8:18)

Utukufu una Yeye KRISTO, Milele na Milele; AMINA.

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *