Home 2022 January 05 Inunue Kweli na Usiiuze!

Inunue Kweli na Usiiuze!

Inunue Kweli na Usiiuze!

“Inunue kweli, wala usiiuze; Naam, hekima, na mafundisho, na ufahamu” (Mithali 23:23)

Kila Mkristo wa kweli anapaswa kuelewa kwamba ukweli unagharimu. Ikiwa hufikiri hivyo, jaribu kulifanya jambo hilo liwe lako wewe mwenyewe; lithamini, litetee, simama kwa ajili yake, na uone kama halina gharama. Utashangaa kuona, kabla hujamaliza kufanya hilo jaribio, tayari limeweza kukugharimu zaidi ya vile ulivyofikiria – masaa yako ya kujipa raha na kujistarehesha, marafiki na pesa pia, n.k.!

Ndio kusema, ukweli unagharama. Wokovu ni bure kabisa lakini ukweli unagharimu – hasa, ikiwa unautaka kwa ajili yako wewe mwenyewe. Wengi wanajua thamani ya ukweli, ingawa hawako tayari  ‘kuununua’. Hawako tayari kulipa gharama ambayo itawawezesha kusema: “Hiki ndicho ninachokiamini. Hii ndiyo imani yangu.” Ukweli hauna thamani hiyo kwao.

Lakini, kama ulikuwa hujui, Neno la Mungu katika Mithali 23:23 linatuhimiza hivi: “Inunue kweli”! NA WALA HALISEMI, “Inunue kweli kama unaweza kuipata kwa bei punguzo; au usubiri wakati wa bei za promotion.” Hapana, bali “Inunua kweli”! Inunue kwa bei yoyote ile. Kwa nini? Kwa sababu, ina thamani zaidi kuliko kitu chochote unachoweza kukitoa, ili kuipata kweli hiyo.

Na ukisha kuinunua; “usiiuze!” Ni wangapi, kati yetu, wameinunua kweli na kuiuza tena? Kwa kipindi fulani, waliithamini na kuitetea nuru fulani kutoka kwa Mungu, iliyotokana na kweli ya Neno Lake; lakini sasa wameiuza kweli hiyo kwa ‘kitu’ kinachoonekana kwao kuwa ni cha thamani zaidi. Hiki, kinaweza kuwa, labda ni kuwa na amani na watu wengine, au cheo, au umaarufu au faida zingine za kitambo. Waliikubali kiakili tu, haikuweza kuwa sehemu ya kuamini kwao. Haikuweza kamwe kutawala mfumo wa imani zao; wakaitupilia mbali kwa vitu vya kupita!

Watu kama hao wanapaswa kusoma tena na tena ushauri huu wa Roho wa Bwana: “Inunue kweli, wala usiiuze.” Hasemi: “Usiiuze mpaka hapo utakapopata bei nzuri zaidi.” Hapana! Bali anasema: “Usiiuze.” Usiiuze kwa bei yoyote ile. Inunue, bila kujali gharama yake ni kubwa kiasi gani na ukisha inunua na kuwa yako, usiiuze kwa bei yoyote ile na/au wala usizingatie kitu chochote kile.

Ni kwa sababu ukweli unathaminiwa kidogo sana katika enzi hii isiyojali, ndio maana watu wengi wa Mungu wamekosa nguvu za kiroho. Wanayashikilia maoni yao badala ya usadikisho, kwa sababu wamelipa Neno la Mungu lisiloweza kukosewa wala lisilobadilika; nafasi ndogo sana katika maisha yao ya kiroho.

Mungu huwabariki na kuwatumia wale wote ‘wanaoinunua kweli na wala wasiiuze…!

“Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu” (Mithali 4:7)

Utukufu Una Yeye Milele na Milele; Amina.

Author: Festus Patta

4 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *