Home 2021 December 26 Ni Nani Atakayetutenga Na Kristo?

Ni Nani Atakayetutenga Na Kristo?

Ni Nani Atakayetutenga Na Kristo?

“Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo?” (Warumi 8:35)

Kumekuwa na watu ambao wanadhani mafundisho juu ya ‘usalama wa milele’ wa muumini katika Kristo kuwa ni uzushi wenye hatari. Wanapinga kila Andiko juu ya suala hilo na kulikanusha. Lakini katika kila moja ya hoja hizo, ukweli huu mkuu, “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo”, ndio unaohitimisha hoja zao.

Ni muhimu kutambua kwamba Mtume Paulo kamwe hatuambii kuhusu upendo wake kwa Kristo, bali daima anatuambia juu ya upendo wa Kristo kwake na kwa wengine (mimi na wewe)! Sheria ya Musa inasema hivi: “Mpende Bwana Mungu wako”, lakini neema ya Kristo inaiweka njia nyingine, ikituambia jinsi Mungu anavyotupenda kupindukia – na upendo huu ndio unaoleta upendo ‘mrejesho’. Mtume Paulo alipata maumivu ya kukatisha tamaa ambayo pengine yangeweza kumfanya aache kazi ya Bwana zaidi ya mara elfu moja, lakini hakuweza kufanya hivyo. Kwa nini? Yeye anasema, “Upendo wa Kristo watubidisha” (2 Wakorintho 5:14); hilo lilimbeba, kama kubebwa na wimbi kali/kubwa lenye nguvu. Bila shaka alikuwa ametawaliwa na jambo hili akilini mwake wakati akiendelea kuandika katika Warumi 8.

“Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa” (Mstari wa 36)

Kwa hivyo alishindwa? La hasha!

“Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda” (Mstari wa 37)

Sio tu kwamba tunashinda vita; bali sisi ni “zaidi ya washindi”, kwa sababu shida hizi hutumika kutuvuta katika ushirika wa karibu zaidi na Yeye, na hivyo kuimarisha uzoefu wetu wa Kikristo.

Wakati watu au mataifa yanashiriki katika vita, kwa ujumla hakuna mtu anayeshinda; Wote wawili wanapoteza. Lakini uzoefu wa kibinafsi wa Mtume Paulo hutumika kama mfano wa kwanza kwamba katika maisha ya Kikristo, “dhiki, shida, mateso, njaa, uchi, hatari [na] upanga” hutuletea zaidi ya ushindi pale tulipozaliwa kwa ajili yake ambaye anatupenda.

Hivyo, Sura hii kuu inafungua na “hakuna hukumu” na inafunga na “hakuna kitakachotutenga”, na Mtume Paulo, anazikusanya nguvu zote za asili pamoja, ikiwa ni wakati, nafasi, au jambo, anatangaza kwamba hakuna hata moja kati ya hayo liwezalo kututenga na “upendo wa Mungu, ambao [unadhihirishwa] katika Kristo Yesu” (Mstari wa 38-39). Iwe ni kifo au uzima, wakuu wa anga, vitu vilivyopo au vitu vijavyo, kirefu au kipana au kitu kingine chochote kilichoumbwa – hakuna hata kimoja kati yavyo, wala katika umoja wavyo – kiwezacho kutishia usalama wetu au kututenga na upendo wa Mungu, ambao ametuonyesha katika Kristo Yesu.

“Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” (Warumi 8:31-39)

Utukufu Una Yeye Milele na Milele; Amina.

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *