Home 2021 December 09 Ni MIMI, Msiogope!

Ni MIMI, Msiogope!

Ni MIMI, Msiogope!

“Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni MIMI, msiogope.” (Marko 6:50b)

Walidhani kuwa wameona mzimu…!

Wakiwa tayari wamechoka kwa “taabu na kupiga makasia” kuukabili upepo wa “kinyume” – upepo wa mbisho, huku bado wakiwa “katikati ya bahari” na usiku ukiwa umeenda sana; waliona kitu kwa mbali ambacho kiliwaogopesha zaidi hata kuishinda ile hofu ya dhoruba waliyokuwa nayo usiku ule.

Walimwona akitembea juu ya bahari, walidhani kuwa ni ‘kivuli’ na woga wa kutisha ukawashika pale ilipowalazimu kukabiliana na jambo ambalo hawakuwahi kukumbana nalo hapo awali. Mwanzoni, bila shaka, walikuwa wamefadhaika na kushikwa na woga usio na kifani. Kisha “wakapiga yowe”, pengine kuomba msaada au kutokana na  kushindwa kujua cha kufanya; na kwa kuitikia yowe hilo, sauti yenye kuwatia moyo ikaja kutoka kwa Bwana wao aliyebarikiwa: “Jipeni moyo: ni mimi; msiogope”!

Tukio lililokuwa limewajaza hofu kuu, likawa limegeuka na kuwa ni Bwana Mwenyewe; ambaye walikuwa wanampenda sana kuliko mwingine yeyote hapa duniani. Tazama nyuso zao! Muonekano wa hofu ukawa sasa umewaacha na sura zao zikawa zimejaa furaha na matumaini. Nyuso zao sasa zimejaa tabasamu…

Je! Kuna funzo lolote ambalo watu wa Mungu tunaweza kulipata hasa tukiwa katika nyakati za taabu? Wakati tukishikwa na hofu au woga upitao kiwango cha imani yetu, na hivyo kushindwa kukabiliana na kile kinachoonekana kuwa kikubwa mbele yetu! Ni heri iliyoje kusikia sauti Yake wakati kama huo, ikisema, “Ni MIMI”; sio tu “niko hapa pia”, bali “Ni MIMI” – “Niko katika shida hiyo ambayo wewe unaogopa kukabiliana nayo. Hakika, Ni MIMI ndiye utakayenipata katika shida zako zote kama utaziangalia kwa ukaribu zaidi.”

Kwa wale ambao ni ‘wazembe’ kiasi kwamba wanachanganya ‘msimamo wa mwamini’ na ‘hali na uzoefu wake’ wanapaswa kuzingatia kwamba ni Mtume Paulo, ndiye ambaye anaandika juu ya ‘nafasi yetu katika ulimwengu wa roho’, ambaye amesema maneno haya katika waraka wake wa mwisho kabisa na katika sura yake ya mwisho:

“Katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha… Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu…” (2 Timotheo 4:16,17)

Lilikuwa ni jambo la kutisha kusimama kama Mkristo mbele ya yule ‘dubwana’, Nero! Na kwa kusimama mbele yake, peke yako – ukiwa umeachwa na wote, lilikuwa ni jambo linaloongeza kukosa matumaini na lilikuwa linazidisha woga. Ah, lakini katika saa yake hii ya giza zaidi “Bwana alisimama pamoja naye, akamtia nguvu”. Ni kweli, Mtume Paulo alijua jambo fulani kuhusu hilo, na sisi pia; tunaweza kuwa na ujasiri huo wakati matatizo yanapojitokeza. Hivyo basi, tunaweza kuyasikia maneno haya yenye kututia moyo na kutufariji: “JIPENI MOYO: NI MIMI; MSIOGOPE”.

Utukufu Una Yeye Milele na Milele; Amina.

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *