Home 2021 November 10 Je! Tunaelewa Tunachokisoma?

Je! Tunaelewa Tunachokisoma?

Je! Tunaelewa Tunachokisoma?

Hili ndilo swali ambalo Filipo alimwuliza mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka alipokuwa ameketi garini mwake akisoma chuo cha unabii wa Isaya (Matendo 8:30), na ni swali ambalo tunapaswa kujiuliza sisi leo, kila wakati tunaposoma Maandiko Matakatifu.

“Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo. Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?” (Matendo 8:27-30)

Daima kuna watu miongoni mwetu, watu wa Mungu, ambao hawajali kabisa kujua kama kile wanachokisoma wanakielewa au la, isipokuwa tu kama kinawachangamsha mioyo yao – BASI!

Kwao Biblia ni kama hirizi ya kiroho, hirizi yenye ‘uvuvio’. Wakichukuamo humo, Maandiko yale tu yanayowavutia, na kuyaacha mengine yasiyowavutia, na hivyo kujiona ni wa kiroho sana na mara nyingi huzungumza juu ya kuiamini kwao Biblia bila kujali kama wanaielewa au la! Lakini “hali ya u-kiroho” kama hiyo, sio ya kweli, na “imani” ya namna hiyo ni ‘imani-kipofu’ na ni ushirikina wa kiwango cha juu!

Ingawa ni kweli kwamba Biblia inatufundisha kweli nyingi ambazo tunaziamini, na ambazo zipo juu ya ufahamu wetu, lakini je! tunawezaje kuamini kile Biblia inachosema kama hatujaelewa hicho Biblia inachosema? Mungu anatutaka tuelewe kile tunachokisoma na kuamini kwa ufahamu wetu ‘wenyewe’ (na sio kupitia ufahamu wa jirani). Kimsingi, imani ya kweli inatutaka tufahamu na tuelewa zaidi na zaidi Neno la Mungu, kama lilivyoandikwa kwenye Biblia zetu.

Mtu ambaye hajali kama anaelewa au haelewi kile ambacho Mungu amesema katika Neno lake, huyo hana nia ya kweli ya kujua kile ambacho Mungu amekuwa akituambia, hata kidogo! Imani yake imejengeka juu ya mapenzi yake yeye mwenyewe badala ya Neno la Mungu, kwa kuwa bila kujali maana ya Maandiko, atachukua kifungu chochote kinachopatana na mapenzi yake na kukitumia apendavyo.

Mungu Mwenyewe, ameweka msisitizo mkubwa juu ya umuhimu wa kuelewa Neno Lake! Wakati fulani, Bwana wetu alipoona umati wa watu, “akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi” (Marko 6:34).

Na sasa, kwa kuwa siri ya mpango mkuu wa Mungu imefunuliwa kwetu, kuna sababu nyingi zaidi za kujifunza Maandiko Matakatifu kwa nia ya kuyaelewa! Ndio maana Paulo, kwa Roho Mtakatifu, amesisitiza jambo hilo anapoandika juu ya maombi yake kwa ajili ya watakatifu:

“MUNGU wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, AWAPE NINYI ROHO YA HEKIMA NA YA UFUNUO KATIKA KUMJUA YEYE;

“MACHO YA MIOYO YENU YATIWE NURU, MJUE TUMAINI LA ​​WITO WAKE JINSI LILIVYO …” (Waefeso 1:17,18)

Kwa Utukufu Wake Kristo Yesu

Author: Festus Patta

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *