Home 2021 July 13 Kuhesabiwa Haki BURE!

Kuhesabiwa Haki BURE!

Kuhesabiwa Haki BURE!

Mungu anatuambia katika Neno lake kwamba waaminio “wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu” (Warumi 3:24). Neno “bure” hapa, halimaanishi “bila gharama,” bali “bila sababu.” Neno lile lile la asili δωρεάν (dōrean) limetafsiriwa hivyo katika Yohana 15:25, ambapo tunayapata maneno haya ya Kristo: “Walinichukia bure.”

Hivyo, wenye dhambi walimchukia Kristo “bila sababu,” lakini Mungu, yeye huwahesabia haki wenye dhambi “bila sababu.” Je! Jambo hili linawezekanaje? Hebu tuone:

Je! Kristo alikuwa amefanya jambo gani mbaya hata limjengee uadui na wanadamu? Hakufanya chochote! Alikuwa ni mwema, alikuwa akiwasaidia wale walio katika shida mbalimbali, aliwaponya magonjwa yao, aliwafanya mabubu waongee, viziwi wasikie, vipofu waone, na vilema waruke-ruke kwa furaha. Lakini ni kwanini basi, walimchukia? Biblia inasema walimchukia “bila sababu, yaani, bila sababu yoyote iliyotoka kwake (iliyo sababishwa na yeye). Sababu ya chuki yao ilikuwa ni kutoka katika mioyo yao mibaya (hao waliomchukia).

Lakini kwa upande mwingine, je! Wakosefu wamefanya nini hata wakastahili kuhesabiwa haki mbele za Mungu? Jibu tena ni kuwa: Hakuna chochote! Wenye dhambi wamevunja amri zake kila siku, wamekuwa wadanganyifu, wezi, wasengenyaji, wazinifu, wagomvi na wanafanya mamia ya dhambi mbalimbali kila uchwao. Lakini kwa upendo, Mungu alimtoa Mwanawe wa pekee aje afe kwa ajili yao pale Kalvari “ili yeye awe mwenye haki na [wakati huo huo] awe mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu” (Warumi 3:26). Mungu, anawapenda na kuwahesabia haki waumini “bila sababu”, yaani, bila sababu yoyote njema ndani yao hao waaminio. Sababu ya Mungu kufanya hivyo, inapatikana katika moyo Wake; yeye mwenyewe, wenye huruma, kwa kuwa “MUNGU NI PENDO.”

Hivyo, wale wanaomtumaini Kristo, ambaye alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, wanahesabiwa haki bila sababu, kwa neema ya Mungu, kupitia ukombozi ulio katika Kristo Yesu.

“Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi” (Warumi 5:8)

“Basi, na ijulikane kwenu, ndugu zangu, ya kuwa kwa huyo mnahubiriwa msamaha wa dhambi; na kwa yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza kuhesabiwa haki kwa torati ya Musa” (Matendo 13:38-39)

Kwa Utukufu Wake Yesu Kristo

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *