Home 2021 June 30 Kwanini Mungu Aliumba Vitu Vyote?

Kwanini Mungu Aliumba Vitu Vyote?

Kwanini Mungu Aliumba Vitu Vyote?

Wakati Mungu aliviumba vitu vyote kwenye Mwanzo 1, haikuwa ni kwa bahati mbaya wala haikuwa bila kusudi lolote.

Mungu alikuwa na mawazo mapema na ya mbali sana. Alikuwa na kusudi. Hata hivyo, wakati ule Mungu alipoviumba vitu vyote hivyo katika Mwanzo 1, hakuonyesha ni kwa nini alifanya hivyo mpaka baadaye.

Tunasoma katika manabii kwamba aliumba kila kitu kwa utukufu wake; lakini je! Uumbaji wake huo unamtukuza Yeye? Je! Ulimwengu ulioharibiwa na uovu na dhambi unawezaje kumletea Mungu utukufu?

Mungu alilificha kusudi lake hilo la uumbaji kuwa siri kwa maelfu ya miaka!

Mungu aliufunua ujuzi wa dhambi, utakatifu, na hukumu ya haki katika vitabu vya sheria kwa Israeli, lakini kusudi lake la umilele la kwanini aliviumba vitu vyote lilifichwa kuwa siri tangu ulimwengu ulipoanza.

Lakini Mtume Paulo anaandika kuwa, siri hiyo iliyokuwa imefichwa na Mungu, sasa imefunuliwa (Waefeso 3:8-9, 1:9-10):

“Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote”

“Akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo”

Wakati tunasoma juu ya siri ya mapenzi ya Mungu, tunasoma kile kilichokuwa kwenye mawazo ya Mungu kabla ya ulimwengu kuanza katika Mwa 1:1. Siku zote Mungu alikuwa amekusudia vitu vyote viwe ndani ya Kristo, hata kabla ya Adamu kukutana na Hawa.

Ilikuwa ni kabla ya ulimwengu kuanza kwamba Mungu alikuwa na kusudi la kufanya kile kilichohitajika kuokoa uumbaji wake kutoka katika dhambi na kifo ambavyo bila shaka ungevipata:

“Ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele, na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili” (2 Timotheo 1:9-10)

Kabla ya ulimwengu kuanza, Mungu alisema “Iwe nuru” (Mwanzo 1:3).

Pia kabla ya ulimwengu kuanza, katika hekima Yake iliyofichwa, Mungu alikusudia kuangaza nuru ya utukufu wake ndani ya mioyo ya wanadamu yenye giza kupitia injili ya Yesu Kristo:

“Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang’aa toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo” (2 Wakorintho 4:6)

Wakati Mungu alipoumba vitu vyote, na kisha vikageuka kuwa vibaya kwa haraka, haikuwa wazi kabisa kwanini Mungu alifanya hivyo hapo mwanzo.

Lakini sasa siri ya mapenzi yake hayo, imefunuliwa!

Vitu vyote viliumbwa na Yesu Kristo, vitu vyote vimeokolewa kupitia Yesu Kristo, na vitu vyote vitampa Mungu utukufu katika Yesu Kristo:

“Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.” (Warumi 11:36)

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *