Home 2021 May 30 Kutimiza Haki Yote!

Kutimiza Haki Yote!

Kutimiza Haki Yote!

Yohana Mbatizaji aliwabatiza Wayahudi kwa maji.

Ubatizo wa maji haukuwa jambo geni kwao. Wayahudi walikuwa wakibatizwa kwa maji kwa karne nyingi chini ya mahitaji ya sheria katika hekalu na katika mabwawa makubwa kama Bethesda (Yohana 5:2).

Hata hivyo, Yohana alikuwa ni wa kipekee kwa sababu alikuwa nabii, hakuvaa mavazi ya hekaluni (alivaa nywele za ngamia), na alikuwa akihubiri nyikani na sio karibu na hekalu.

Alihubiri ubatizo wa maji na toba kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Ondoleo la dhambi ni msamaha wa dhambi:

“Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi” (Marko 1:4)

“Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi” (Luka 3:3)

Ubatizo wa Yesu

Wakati Yesu alipokuja kubatizwa kwa maji, Yohana alitambua kuwa Yesu hakuwa na dhambi ya kusamehewa, na hivyo akamkataza Yesu kubatizwa:

“Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?” (Mathayo 3:14)

Yesu alisisitiza kubatizwa, lakini sio kwa sababu alikuwa na dhambi za siri/zilizojificha za kutubu! Yesu alijua kuwa yeye alikuwa ni Mungu aliyejidhihirisha katika mwili, na hakuwa na dhambi. Haya yalikuwa ndiyo maneno yake kwa Yohana Mbatizaji:

“Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali” (Mathayo 3:15)

Sababu ya Yesu kuhitaji kubatizwa kwa maji na Yohana pamoja na Israeli mwenye dhambi haikuwa kwa sababu alikuwa na dhambi za siri za kuungama, lakini ilikuwa ni kwa ajili ya kutimiza haki yote.

Lakini, hiyo ilikuwa inamaanisha nini?

Ili Kutimiza Sheria

Yesu hakuja kuharibu ahadi, manabii, wala sheria walizopewa Israeli. Hakuwa akiweka muundo mpya wa ubatizo wake wa maji, bali alikuwa akiutimiza ule wa zamani:

“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza” (Mathayo 5:17)

Kuoshwa kwa maji kulihitajika kwa watu wengi tofauti kwa nyakati tofauti na kwa malengo tofauti chini ya sheria. Kama mtu alishindwa kufanya hivyo, alikuwa na hatia ya kuvunja sheria.

Sheria moja ambayo ilikuwa ikitumiwa na Yohana Mbatizaji ilikuwa ni sharti la kuoshwa kwa makuhani wote.

Yohana alikuwa akihubiri ufalme uje na katika ufalme taifa lote la Israeli lingekuwa makuhani kwa Bwana (Kutoka 19:6, Isaya 61:6).

Yesu aliishika sheria kikamilifu, na kwa hiyo alijitiisha kwa kanuni zinazohitajika ili kutimiza haki yote.

Kutimiza Manabii

Sheria na manabii walizungumza juu ya Yesu. Unabii kadhaa ulinena juu ya mjumbe kuja kabla ya Bwana kuandaa njia yake:

“Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako. Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake” (Marko 1:2-3)

Yohana Mbatizaji alikuwa mjumbe huyo, na Yesu alikuwa ndiye Bwana aliyetabiriwa.

Mungu alimpa unabii Yohana Mbatizaji kwamba yeye angeweza kumtambua Masihi kupitia ubatizo wake wa maji:

“Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji. Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu” (Yohana 1:31-33)

Kama Yesu asingetimiza yaliyosemwa/yaliyotabiriwa juu yake, basi unabii ungekuwa umebatilika, ujumbe wa Yohana Mbatizaji ungekuwa ni wa uwongo, na Mungu hangekuwa mwadilifu.

Yesu alikuja kuwakamilisha manabii na alitimiza unabii mwingi kwa kubatizwa kwako kwa maji na Yohana.

Ili Kuhalalisha Ujumbe wa Yohana

Yesu alibatizwa kwa maji ili kuhalalisha ujumbe wa Yohana.

Yohana Mbatizaji alihubiri kwamba ufalme ulikuwa karibu. Wale wote waliosikia mahubiri yake na kulipokea neno la Mungu kwake walibatizwa kwa maji (kama vile walivyomuhesabia haki Mungu katika huduma ya Yesu):

“Na watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohana” (Luka 7:29)

Kwa kubatizwa na Yohana, Yesu alikuwa anasema, “Mafundisho ya Yohana ni kweli yametoka kwa Mungu”.

Ili kujipanga katika unabii wa Mungu na ujumbe wake, Yesu alihitaji kubatizwa kwa maji na Yohana.

Kupitia kushiriki kwake katika ubatizo wa maji wa Israeli mwenye dhambi, Yesu alijitambulisha (identified) na Israeli akiutarajia ufalme ufike, kisha akajionyesha yeye mwenyewe kuwa ndiye atakayeitimiza haki yote.

Ili Kujitambulisha

Mara nyingi, katika wakati wa Yesu hapa duniani, Mungu aliongea kutoka mbinguni na kushuhudia kwamba Yesu alikuwa ni Mwanawe aliyependezwa naye (Mathayo 17:5):

“Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye”

Yesu alitambua kwamba yeye alikuwa ni Mwana wa Mungu (Luka 2:49), na kwamba ubatizo wake wa maji ungemtambulisha yeye kwa Israeli. Ndio maana, Yesu alimsisitiza Yohana ambatize kwa maji.

Alipopanda kutoka majini kubatizwa, Roho wa Mungu alishuka juu yake na Mungu alizungumza ili kila mtu asikie:

“Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye” (Mathayo 3:16-17)

Kama pasingekuwa na ubatizo huu wa maji wa Yesu, pasingekuwa na utambulisho huu wa hadharani ambao Mungu aliufanya ili kumtambulisha Yesu kwamba alikuwa ni Mwana wa Mungu.

Yohana Mbatizaji, baadaye alilihubiri tukio hili kuwa uthibitisho kwamba yeye Yesu alikuwa ndiye Masihi:

“Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu. Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu” (Yohana 1:32-34)

Hitimisho

Hakuna mtu yeyote katika wakati wa Yesu ambaye angeweza kutimiza kile Yesu alichokifanya katika ubatizo wake wa maji. Na wala hayuko mtu yeyote leo, katika kipindi hiki cha neema, mwenye haja ya kumfuata Yesu katika ubatizo huo. Tunao ubatizo mkubwa zaidi ambao unatutambulisha/unatuunganisha na Kristo, tukibatizwa kwa imani katika kifo chake:

“Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe!” (Luka 12:50)

“Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?” (Warumi 6:3)

Yesu hakubatizwa kwa maji ili anzishe agizo jipya. Ubatizo wa maji ulikuwa ni “mila” ya zamani ya Wayahudi.

Yeye hakubatizwa kwa maji kwa sababu ya ondoleo la dhambi zake, kama vile ilivyokuwa kwa watu wengine ambao walibatizwa kwa ubatizo wa maji.

Alibatizwa kwa maji ili kutimiza haki yote kwa sababu yeye alikuwa ndiye Masihi aliyetabiriwa, Mwana wa Mungu.

Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *