Home 2021 April 06 IMANI katika Nini?

IMANI katika Nini?

IMANI katika Nini?

Wakati mwingine watu huuliza, “Je! Imani inatosha kwa wokovu?” Au, Je, wewe “unayo imani?”

Lakini, swali linabaki kuwa ni “Imani” katika nini? Kwa sababu hakuna kitu maalum juu neno ‘imani’ lenyewe peke yake.

Kila mtu anajifikiria kuwa ni mtu wa imani, lakini ni imani katika nini?

Kila dini ya uwongo ina watu wa imani, lakini ni imani katika nini?

Kila mtu anayeenda kanisani, hata yule asiyejua Biblia, anasema yeye ni mtu wa imani, lakini ni imani katika nini?

Ni kile ‘kitu’ kinachobeba imani yetu ndicho ambacho hufanya imani kuwa dhaifu au kuwa imani yenye nguvu!

Imani isiyo na msingi katika ukweli haina nguvu…

Imani katika kitu kibaya haikubaliki…

Imani bila ya ‘kitu cha kukiamini’ sio imani kamwe, bali ni ujinga…

Kuwa na imani tu hakuna maana yoyote, isipokuwa imani hiyo ipo katika ‘kitu’ sahihi. Kitu sahihi siku zote ni kile ambacho Mungu amekitoa kama lengo la imani.

Msadifishaji wa Wasiomcha Mungu

“Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki” (Warumi 4:5)

Takribani kila dini hufundisha kwamba kuhesabiwa haki mbele za Mungu, ni lazima tujidhibitishe sisi wenyewe kuwa ni wenye haki.

Imani ya kila ‘mtu wa dini’ haina maana ikiwa anaamini kuwa watu wasiomcha Mungu hawawezi kuhesabiwa haki mbele za Mungu.

Kwa kweli, ukosefu wa utauwa ni mbaya na, katika haki, unalaaniwa na Mungu na wanadamu pia; lakini Mungu ameweka namna/njia ya kuwahesabia haki watu wasiomcha Mungu bila matendo yao mema…

Kama imani yako ‘inajinyonganyonga’ na kufadhaika katika kuukubali ukweli huu, basi imani yako haikubaliki mbele za Mungu; ndiyo kusema huna imani katika injili iokoayo.

Tathmini yaliyomo (yaliyobebwa) kwenye imani yako, unaweza ukaona kuwa ni imani juu yako wewe mwenyewe na juu ya utauwa wako, badala ya kipawa (utoaji) wa Mungu.

Mungu anaweza kuwahesabia haki watu wasiokuwa watauwa ambao wemeiweka imani yao katika damu ya Yesu Kristo kama malipo kamili ya dhambi zao zote.

Imani katika Kifo na Ufufuo

“Bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki” (Warumi 4:24-25)

Ikiwa imani yako haijumuishi ufufuo wa Yesu Kristo kwa niaba yako, ambayo ni kazi iliyomalizika, kamilifu na timilifu ya Kristo Yesu, basi imani yako ni bure:

“Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu” (1 Wakorintho 15:17)

Walakini, haki inaweza kuhesabiwa kwetu ikiwa tunaamini katika Mungu ambaye alimtoa Kristo kwa ajili ya makosa yetu, na akamfufua ili tupate kuhesabiwa haki.

“Watu wengi wa imani” wanadhihirisha kutokujua juu ya jinsi Mungu anavyowaokoa, au kwamba imani yao imejengeka (hupatikana) katika matukio (mazingira), au “katika miujiza ya kila siku”. Hii sio imani ambayo Mungu anaiheshimu.

Imani hutokana na kusikia neno la Mungu (Warumi 10:17). Pamoja na ukweli huo, pale Biblia inaposema tuwe na imani, ni lazima tuulize, “ni imani katika nini?”

Sio watu wote katika Biblia walikuwa na imani katika kitu kimoja. Imani katika agano, sheria, ufalme uje, au hata jina la Mwana wa Mungu sio ‘yaliyomo’ kwenye injili leo.

Imani katika ‘kazi’ ya Kristo kwa niaba yetu ndicho ‘kilichotolewa’ (kinachotakiwa kuaminiwa) kwa ajili ya imani yako. Sio imani katika jambo lolote la ‘maana’, bali ni imani katika jambo ‘sahihi’: imani katika injili ya leo!

Amini Injili

“Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko” (1 Wakorintho 15:1-4)

Bila kifo na ufufuo wa Kristo imani ya Kikristo ni upofu, haina nguvu ya kuokoa, ni ya kijinga, na haikubaliki mbele za Mungu. Hii ndiyo sababu Paulo anasisitiza sana juu ya mahubiri ya msalaba kama kitu cha msingi katika imani yetu.

Ikiwa imani hii inayotokana na fundisho lenye uzima inakufanya usifurahi, au inapingana na kile unachofikiri kuwa Mungu anapaswa kukibali, basi imani yako haitegemei fundisho la Biblia, na haijajengeka juu ya kweli ya kibiblia.

Watu wanaamini miujiza, lakini wanaweza kukataliwa watakapokufa.

Watu wanaamini malaika, na matendo mema, lakini watakuwa na hatia siku ya hukumu.

Watu wana imani katika ubinadamu, mapenzi mema, na upendo, lakini hawataokolewa kwa sababu wao wamekikataa kipawa cha Mungu.

Tumeokolewa kwa kuamini injili ya wokovu wetu, sio kuwa na imani katika hisia, makanisa, mifumo ya kidini, kazi nzuri, bidii, kwenda kuwatembelea wajane na yatima, malaika, miujiza, au kuwa na imani katika yoyote kati ya mamilioni ya vitu ‘watu wa imani’ wanavyoviamini.

Injili ya wokovu wetu ni kazi iliyokamilishwa ya Kristo Yesu kwa niaba yetu (Efe1: 13):

“Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu.”

Jambo moja tu linaokoa. Imani moja tu inakubalika. Imani moja tu ndiyo iliyofundishwa na Mtume Paulo kama INJILI. Hiyo ni imani katika kifo cha Kristo kwa ajili ya dhambi zetu, kuzikwa kwake katika mwili, na ufufuko halisi ili kutupatia uzima wa milele.

Kazi ya msalaba ya Kristo ndiyo inayookoa. Je! Imani yako ni hiyo?

Kwa Utukufu wa Jina lake Kristo Yesu!

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *