Home 2020 September 18 Tunaokolewa katika Nyakati Tatu

Tunaokolewa katika Nyakati Tatu

Tunaokolewa katika Nyakati Tatu

Tumeokolewa, Tunaokolewa, Tutaokolewa

Kauli hii inaweza kuonekana kuwa jambo lililo dhahiri, lakini kile kilicho dhahiri kwa baadhi ya watu, huwa hakiko hivyo kwa watu wengine.

Nyakati Tatu za Wokovu

Maandiko yanasema juu ya kuokolewa kwetu katika nyakati tatu tofauti. Katika sehemu moja maandiko yanasema kwamba “tumeokolewa” (yaani zamani – wakati uliopita). Katika sehemu nyingine maandiko yanasema kwamba “tunaokolewa” (wakati huu wa sasa na ni tendo endelevu) na katika sehemu nyingine maandiko hayo pia yanasema “tutaokolewa” (baadaye – wakati ujao).

Kauli zote hizo tatu ni za kweli. Uelewa juu ya jinsi tunavyookolewa katika hali na nyakati hizo tatu, husaidia sana kuzuia mitizamo isiyofaa juu ya wokovu, wakati huo huo pia inatusaidia kupata ukweli juu ya uhakika wa wokovu.

1. Tumeokolewa (2Timotheo 1: 9) – Wokovu Wetu Uliokamilika

“Ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele

Kuna namna ambayo tayari Mungu amemwokoa kila Mkristo. Katika maana hii, wokovu una maana ya msamaha wa dhambi (Kuhesabiwa Haki).

  • Anania alimwambia Paulo, “Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako” (Matendo 22:16). Kwa hivyo Paulo, mara tu alipotii, dhambi zake zilisafishwa. Aliokolewa!
  • Paulo aliwaambia Wakorintho, “mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki … “(1Wakorintho 6:11). Waliokolewa!
  • Paulo anazungumza juu ya Mungu Mwokozi wetu, “alituokoa…” (Tito 3:4-5). Wakati uliopita (jambo timilifu), sivyo?
  • Mapema kabla, kwenye hiyo hiyo Tito, Paulo anasema, “Neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa” (Tito 2:11).

2. Tunaokolewa (1Wakorintho 1:18) – Wokovu Wetu wa Sasa

“Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu”

Kuna namna ambayo bado Mungu anamwokoa kila Mkristo. Katika maana hii, wokovu ni sawa na ukuaji wa Mkristo na uvumilivu (Kutakaswa).

  • Paulo aliongea na Wakorintho juu ya “wale ambao wanaokolewa” (2Wakorintho 2:15). Hapa hatuna wakati uliopita, bali wakati uliopo (sasa) – Paulo anazungumzia juu ya jambo linalofanyika wakati uliopo. Tunalo neno “kuokolewa” likiwa limetumika katika wakati wa sasa, katika hali inayoendelea.
  • Paulo anawaambia Wafilipi, “utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka, kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu … ” (Wafilipi 2: 12-13). Hapa tunaona wokovu ukiwa umewasilishwa kama kitu kinachofanyiwa kazi na sisi wenyewe tukiwa katika ushirikiano na Mungu. Inaonyesha kuwa ni kama jambo lisilokamilika bado, kuna kazi ya kufanywa.
  • Tafakari maana ya swali hili, “Sisi Je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii?” (Waebrania 2:1-3).
  • Kauli nyingine inayoelezea hilo ni hii, “Jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu… ” (2Petro 1:10).
  • Yohana anasema kwamba “damu yake Yesu, yatusafisha dhambi yote…” (1Yohana 1: 7). Dhambi zetu za zamani zilisamehewa wakati ule tulipokuwa Wakristo (tulipookoka), lakini dhambi zile tunazofanya tangu wakati huo, zinahitaji kupata msamaha pia. Msamaha na wokovu vinaendelea tunapotembea katika nuru.

3. Tutaokolewa (Warumi 5: 9-10) – Wokovu Wetu Ulioahidiwa

“Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake”

Kuna namna ambayo Mungu ataokoa watu hapo baadaye (wokovu ni tukio la baadaye). Kwa maana hii wokovu ni sawa na kuja kwa Kristo mara ya pili (kutukuzwa kwetu).

  • Yesu alisema, “Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele” (Mathayo 25:46). Hili ni tukio la baadaye.
  • Kama tulivyoona kwenye utangulizi hapo juu, Paulo amesema mara mbili, “Tutaokolewa …” (Warumi 5: 9-10). Hili halihusiani na yaliyopita (ya zamani) wala ya sasa, bali yajayo (ya baadaye); sivyo ilivyo?
  • Paulo anatoa taarifa ya kufurahisha, “Kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini” (Warumi 13:11).
  • Roho Mtakatifu ametolewa “kama dhamana (arabuni) ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake … “(Waefeso 1:14). Hapa ukombozi na urithi wa milele ni kitu cha kutazamiwa, kitu cha baadaye.
  • Paulo anazungumza juu ya “tumaini la wokovu” (1Wathesalonike 5: 8). Tumaini la wokovu inamaanisha wokovu ni wa baadaye. Kama wokovu wetu ungekuwa umekamilika kabisa, umemalizika; basi kungekuwa hakuna haja ya kuushikilia kama tumaini letu.

 Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

4 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *