Home 2020 September 09 Kwanini Tunafanya Uinjilisti?

Kwanini Tunafanya Uinjilisti?

Kwanini Tunafanya Uinjilisti?

Ni lazima tufahamu sababu zinazotufanya twenda kufanya uinjilisti. Hapo chini nimejaribu kuorodhesha baadhi ya sababu kubwa na za muhimu ingawa najua kuna sababu zingine nyingi zaidi katika Maandiko Matakatifu.

Kumpendeza Mungu na kuonesha upendo wetu kwake

Tunaposoma Maandiko tunagundua kwamba kushuhudia Habari Njema kunampendeza Mungu. Yohana 15:8 inaeleza kwamba Mungu hutukuzwa wakati tunapozaa matunda. Vilevile, 2 Wakorintho 5:9 inaeleza kwamba popote tulipo shabaha yetu iwe ni kujitahidi katika kumpendeza Mungu. Zaidi ya hayo Mungu alimwuliza nabii Isaya, “Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?” Ndipo Isaya akajibu, “Mimi hapa, nitume mimi” (Isaya 6:8). Naamini kwamba Mungu hupendezwa sana tunapojitoa ili tutumwe kushuhudia kwa niaba yake Mungu. Hii inamaanisha tumeungana naye katika kuuokoa ulimwengu. Kwa hiyo, sababu yetu ya kwanza kufanya uinjilisti ni kwamba kushuhudia humpendeza Mungu na kumwonyesha upendo wetu kwake.

Tuliagizwa kueneza Injili

Paulo aliyeupokea ufunuo maalum kutoka kwa Kristo Yesu aliweza kutuagiza tuieneze huduma au neno la upatanisho katika 2 Wakorintho 5:18-20:

“Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu”

Naamini kwamba hilo ndilo agizo la mwisho kwa wafuasi wake Kristo (na kwa wakati huu) watangaze kuhusu Kristo na kazi yake ya kuwapatanisha wanadamu na Mungu kwa njia ya mauti yake msalabani. Vilevile hata Yesu Kristo aliagiza wanafunzi wake waende wakayafanye mataifa yote kuwa wanafunzi katika Mathayo 28:18-20 (Marko 16:15-18):

“Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya”

Kwa hiyo basi, sisi kwa agizo lo lote tutakalolishika, tunajikuta kwamba tunapaswa kuieneza Injili!

Upendo wa Kristo Unatubidisha

Katika 2 Wakorintho 5:14 twasoma kwamba “upendo wa Kristo watubidisha”. Halafu vifungu vinavyofuata vinaeleza kuhusu huduma hiyo ya upatanisho; jinsi Kristo alivyotupenda na kujitoa kwetu. Tunapaswa nasi tuwapende wengine na kujitoa kwa ajili yao (1 Yohana 3:16). Vilevile, Paulo alitamka katika 1 Wakorintho 9:16 kwamba, “Ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!” Paulo aligundua jinsi alivyokuwa kabla hajakutana na Kristo naye alisukumwa na upendo wa Kristo kuwahubiria wengine.

Mungu Hutumia Wanadamu

Ni ajabu kwamba Mungu, mwenye nguvu nyingi na uwezo mkubwa wa kuokoa, alichagua kuvitumia vyombo vilivyo dhaifu kama wanadamu. Mungu angeweza kuwaendea wapotevu kwa njia mbalimbali nyingine. Kwa mfano angeweza kuwatumia malaika, ishara, maono, maandishi ukutani (kumbuka Danieli), sauti ya wanyama (kumbuka Balaamu), au sauti kutoka mbinguni (kumbuka Ubatizo wa Yesu). Lakini mpango wa Mungu kwa leo ni kuitangaza Injili yake akitumia mwanadamu mmoja kumshuhudia mwingine. Chunguza Warumi 10:13-15. Watu hawawezi kuliita jina la Bwana bila kumwamini. Hawawezi kumwamini bila kumsikia. Hawawezi kumsikia bila mhubiri (MWANADAMU). Hawawezi kuhubiri bila kupelekwa (WANADAMU TENA). Ibarikiwe miguu ya wanadamu! Mungu amejitengenezea mpango wa ajabu wa kutuhusisha sisi tusiostahili katika kazi yake ya kueneza Injili.

Uzuri wa Ajabu Mno wa Mbinguni

Kitu kizuri kinastahili kutangazwa. Kama Wakristo wengi zaidi wangetafakari uzuri wa mbinguni kulingana na hali yetu ya hapa duniani, wangejibidisha katika kuitangaza njia ya kufika huko. Maandiko mengi huonesha baraka zote za mbinguni (Yohana 10:10; Efeso 1:3; Zaburi 16:11; Ufunuo 21:4-11, 18). Watu siku hizi wanatumia muda wao mwingi kutafakari na kubuni mbinu za kujisafirisha ili wafike Ulaya na Marekani wakati asilimia 99 hawataenda. Ingekuwa ina maana zaidi kwao kutafuta kwa bidii usafiri kwa safari yao ya mwisho ambayo itawafikisha katika milele ijayo! Mwanadamu huhangaika na dunia kwa ajlili ya ugonjwa, umaskini, na huzuni nyingi. Tuwatangazie watu kuhusu mahali ambapo mambo hayo hayawezi kuwagusa tena. Tuwaelezee kuhusu mbinguni ili watake kuokoka na kwenda huko.

Mateso na Ubaya wa Jehanamu

Kinyume kabisa na sababu ya hapo juu ni kwamba wasipochagua kuufuata uzuri wa mbinguni watakuwa wamechagua ubaya na mateso ya Jehanamu. Watu wangefahamu kikamilifu maelezo ya Maandiko Matakatifu kuhusu Jehanamu wangejishughulisha zaidi ili wajiepushe na hali hiyo. Kwanza Jehanamu ni:

  1. Hukumu na Adhabu – Waebrania 9:27 inaeleza kwamba kila mtu atakufa na baada ya hapo ni HUKUMU. Mathayo 25:46 ineleza kwamba wasioamini “Watakwenda zao kuingia katika ADHABU YA MILELE.” Watu siku hizi hawayaamini Maandiko kwamba Mungu atawahukumu kwa adhabu ya milele. Wanafikiri Mungu atawasamehe tu na hawezi kuwahukumu. Mimi naamini Neno lake Mungu siyo fikira za wanadamu.
  2. Mateso – Mathayo 22:13 inaeleza, “Mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.” Hakuna anayeweza kutamani mahali hapo! Pia katika Luka 16:23-24 tajiri aliyekufa aliomba sana kwa vile aliteswa sana na moto. Hii ni mifano ya kutuonesha hali ya Jehanamu.
  3. Ni ya Milele – Soma Mathayo 9:43 na Ufunuo 14:11; 20:10. Mistari yote hiyo inaeleza kwamba hali hii ya adhabu na mateso ni ya milele. Wengi wanaamini watateswa kwa muda kidogo halafu watu wakiwaombea, basi wataruka kutoka kwenye mateso na kuingia paradiso. Lakini, Neno la Mungu halina tone hata moja la mafundisho kama hayo. Biblia inaeleza dhahiri kwamba kupotea ni kwa milele katika mateso ya ajabu yasiyo koma wala kupungua makali yake. Kazi ya Shetani ni kudanganya na kuugeuza ukweli wa Neno la Mungu ili watu wasiamini.

Naamini sisi Wakristo tungesaidiwa sana katika kufanya uinjilisti wetu kama tungeweza kwenda kukaa mbinguni kwa dakika moja halafu kwenda Jehanamu kwa dakika moja ili tuweze kupata picha kamili ya hali mbili za milele zinazowasubiri wanadamu wote. Tungefanya hivyo tungehubiri kweli ya Injili! Lakini, Biblia imeshatuelezea wazi; kwa hiyo tushuhudie tunavyofahamu kuwa hiyo hali ni kweli kutoka katika Neno la Mungu. Tukifanya hivyo tutakuwa tunafanya kama Yuda alivyosema, “Waokoeni kwa kuwanyakua katika moto” (Yuda 23).

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *