Home 2020 August 28 Uinjilisti wa Mtu kwa Mtu

Uinjilisti wa Mtu kwa Mtu

Uinjilisti wa Mtu kwa Mtu

Kwanza kabisa ni lazima tuelewe kwamba uinjilisti unaofundishwa katika Biblia ni uinjilisti wa mtu kwa mtu na wa nyumba kwa nyumba [personal evangelism].

Ingawa mikutano mikubwa ya injili (Crusades) huonekana kuwa na faida kubwa, watafiti wamegundua kwamba uinjilisti wa mtu kwa mtu una manufaa na matokeo ya kudumu zaidi kuliko mikutano hiyo mikubwa.

Sababu zinazoainishwa ni kama zifuatavyo:

  • Uinjilisti wa mtu mmoja mmoja humlenga mtu mmoja na hugusa mahitaji yake binafsi;
  • Ufuatiliaji wa mtu kwa mtu ni rahisi zaidi;
  • Maswali na vikwazo au changamoto za mtu binafsi ni rahisi kupatiwa majibu katika uinjilisti wa namna hii;
  • Mtu hujisikia huru akiwa nyumbani kwake au katika mazingira aliyo yazoea, hivyo humuwia rahisi kwake kusikia neno la Mungu na kulipokea;
  • Mtu akikubali kupokea injili hukubali kutoka ndani na siyo kukubali kwa sababu ya kushawishiwa na marafiki au kwa kufuata tu mkumbo kama inavyokuwa kwenye mikutano;
  • Hutoa fursa kwa waliomshuhudia kuweza kumfundisha na kumshirikisha vizuri zaidi neno la Mungu;
  • Uinjilisti huo unaweza kufanyika na kila mtu (wanaume, vijana, wanawake, n.k.) na siyo wainjilisti ‘maalum’ peke yao wanaodhaniwa kuwa ndio wenye uwezo wa kuwahubiria watu wengi, tena hadharani.

Mara nyingi uinjilisti unoafanyika siku hizi   hauleti mabadiliko wala maendeleo yo yote katika Mwili wa Kristo. Uinjilisti wa mtu kwa mtu ndio mbadala pekee na ufanya kazi ya kweli na ya kudumu katika nyakati hizi za sasa. Kwa sababu hiyo inatupasa kuwa na miongozo mbalimbali katika kuifanya huduma hiyo.

Uinjilisti wa Mtu Mmoja Mmoja Maana Yake ni Nini Hasa?

Tunaweza kueleza jibu la swali hilo kwa maneno mengi ila kwa urahisi wa kukumbuka, tuigawe maana hiyo katika mambo makubwa mawili:

  1. Kumwelezea mtu mmoja mmoja asiye Mkristo Habari Njema za wokovu.

Uinjilisti wa namna hii unafanyika kwa mtu mmoja au hata wawili lakini siyo kwa kuwakusanya watu wengi na kuanza kuwahubiria. Uinjilisti huo unahusu mambo yanayomfaa mtu asiye Mkristo. Yaani, anayestahili kuinjilishwa ni yule ambaye bado hajampokea na kumkubali Yesu Kristo kama Mwokozi wake na kuokolewa. Aliyeamini na kuokolewa, hata kama siyo mshirika wa dhehebu lako au kanisa lako, hastahili kushuhudiwa wokovu. Siyo kawaida kwa tajiri kuoneshwa njia ya kupata utajiri! Wengi siku hizi hufanya hivyo. Huu siyo uinjilisti, bali ni wivi wa samaki waliokwisha kuvuliwa. Nami nina wasiwasi mkubwa kama kufanya hivyo kunampendeza Mungu! Makanisa na viongozi wangezitumia nguvu zile wanazozitumia kunyang’anyana watu katika kuwashuhudia wale ambao hawajaamini ili waokoke, hakika Mungu angeweza kuleta baraka kuu mno kwa wote!

  1. Ni kumwonesha mtu anayesikia Injili jinsi wokovu unavyotimiza mahitaji yake binafsi.

Katika kuieleza Injili kwa mtu mmoja mmoja ndipo mwinjilisti anaweza kumlenga hasa msikilizaji na mahitaji yake. Kama katika mazungumzo ya kushuhudia unashindwa kuyagundua mahitaji ya msikilizaji wako na kumwonesha kwamba kazi aliyoifanya Yesu Kristo msalabani ni kwa ajili ya kuyatimiza mahitaji hayo, basi huduma yako itakuwa kama kusimulia hadithi za kufurahisha watu tu!

Watu wengi wameshawahi kusikia habari kuhusu Yesu Kristo na hata kufahamu ‘misamiati’ ya mambo ya kikristo, lakini hawajawahi kukutana na Kristo kibinafsi na madai yake kwao. Hawaoni udhaifu wao na kwamba huo unawazuia kumfikia Mungu Mtakatifu mbinguni. Hiyo ndiyo kazi ya mwinjilisti kuwaelezea jinsi hali yao ilivyo na jinsi mahitaji yao yavyoweza kutimizwa ndani ya Kristo Yesu na sadaka yake ya uzima wa milele.

Ndani ya Injili kuna faida nyingi sana. Tafakarii kidogo kuhusu mambo yote yaliyotendeka kwako ulipomkiri Kristo kama Mwokozi wako:

  • Msamaha wa dhambi zako zote (1Yoh 1:9; Efe 1:7);
  • Urithi wa ajabu mbinguni pamoja na Bwana (Efe 1:11; 1 Pet 1:4);
  • Moyo wako ulisafishwa (Zab 51:10);
  • Nguvu za Mungu mwenyewe ziliingia ndani yako katika utu wa Roho Mtakatifu (Rum 8:9, 10);
  • Ulipewa mwanzo mpya (2 Kor 5:17);
  • Ulizaliwa katika familia ya Mungu (Tit 3:5, Yn 1:12);
  • Ulipata tumaini jipya (Efe 1:12; Tit 3:13);
  • Ulitiwa muhuri (kuhifadhiwa) na Roho Mtakatifu mpaka siku ya ukombozi (Efe 1:13, 14);
  • Kazi njema ilianza ndani yako ambayo itamalizika siku ya unyakuo (Flp 1:6);
  • Ulipata njia/uwezo na kibali cha kuwasiliana na Mungu moja kwa moja (Efe 2:18; Ebr 4:16);
  • Uliunganishwa na wote walio ndani ya Kanisa lililo Mwili wa Kristo (1 Kor 12:13; Efe 2:14, 15);
  • Ulipewa uzima tele (Yn 10:10);
  • Ulipewa uzima wa milele (Yn 3:16; 6:47);
  • Ulikwepa ghadhabu ya Mungu (Rum 8:1; Yn 3:36);
  • Ulipata amani na Mungu (Rum 5:1; Efe 1:14);
  • Ulipata sababu mpya ya kuishi (Flp 1:21; Mdo 20:24); n.k.

Kwa kweli wokovu ni utajiri wa ajabu! Utulie, umshukuru na kumsifu Bwana kwa kazi ya njema sana aliyokufanyia!

Sasa unaweza kugundua kwa nini nimeeleza hapo juu kwamba kuna faida nyingi za wokovu. Naamini kwamba faida moja ya wokovu inakufurahisha zaidi wewe kuliko itakavyomfurahisha mtu mwingine, na mtu mwingine ataifurahia faida nyingine tofauti kuliko wewe. Kazi ya mwinjilisti ni kutafuta hali ya mtu na kumshuhudia kulingana na sehemu zile zinazomhusu ili apate kujua faida ya kuokoka. Naamini kwamba watu wengi hawajaitikia wito wa wokovu kwa sababu ‘wainjilisti’ hawajafanya kazi hii ya kumlenga vizuri msikilizaji na ujumbe wao. Badala yake wahubiri hupenda kuongea waliyoyazoea au waliyojifunza ‘shuleni’ bila kumjali wanayemshuhudia na kutambua hali zake mbalimbali. Hii imesababisha kuwepo kwa uinjilisti usio na manufaa). Hima, naomba tuchunguze sana suala hili la uinjilisti linaloyalenga mahitaji na hali ya kila mtu mmoja mmoja. Ndipo hapo tu, tutakapoufurahia uinjilisti wenye Matunda, yaani uletao watu kwa Bwana.

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *