Home 2020 August 20 Kuwafanya Vipofu Waone Kupitia SIRI

Kuwafanya Vipofu Waone Kupitia SIRI

Kuwafanya Vipofu Waone Kupitia SIRI

Kujifunza injili ya Kristo sawa sawa na ufunuo wa ile SIRI, ni uzoefu wa kushangaza, ni jambo linalofumbua macho sana!

Imeshuhudiwa mara nyingi kwamba kujifunza kugawa kwa usahihi “UNABII” na “SIRI” hufanya Biblia iwe “wazi zaidi”, “rahisi kueleweka”, na “yenye kuleta maana”.

Baada ya kukaa “kanisani” kwa kipindi cha miaka 20 hadi 30 hivi, watu walioondoa upofu wao kupitia kujifunza siri, wanashuhudia kwamba kujifunza jinsi ya kuigawa kweli ya neno la Mungu sawa sawa ni kama vioo vyenye matope vikioshwa kwa maji safi.

Watu ambao walikuwa hapo awali wamechanganyikiwa na walikuwa hawajui yale ambayo Biblia inayasema, sasa wanaweza kuelewa na kuona ukweli wa injili.

Paulo Alitumwa Kuwafungua Watu Macho

Fundisho hili lenye kuwafungua watu macho (Kuwafanya Vipofu waone), ndilo hasa lengo la Kristo kumtuma Paulo kuhubiri injili kati ya Mataifa (Waefeso 3:2).

“uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi” (Matendo 26:18)

Paulo alikuwa akiomba wakati wote, bila kukoma, kuwa macho ya mioyo yao (hao aliotumwa kwao) yafunguliwe kwa ile injili ambayo Mungu amempa (ameaminiwa) uwakili wake.

“macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo” (Waefeso 1:18)

SIRI hii ya Kristo inahusu tumaini la utukufu katika ulimwengu wa roho kwa mtu yeyote anayeamini injili ya wokovu.

“ambalo nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu; siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa SIRI hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu” (Wakolosai 1:25-27)

Upofu kwa SIRI

Watu wengi na makanisa mengi pia yamejaa mkanganyiko juu ya injili ya kweli na ni nini Biblia inafundisha na kwa nani. Machafuko haya ya fundisho ni matokeo ya mafundisho ya kishetani na waalimu wa uwongo ambao hawaheshimu SIRI ya Kristo iliyofunuliwa kwa Paulo.

“ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu” (2 Wakorinto 4:4)

“Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote” (2 Timotheo 2:7)

Injili inapaswa kuwa taa/nuru. Ukweli wa kile Mungu anachokifanya leo unapaswa kuwa wazi kwa watu wote, wenye kuweka mambo peupe – bila kificho, ili watu wote wauone ukweli huo.

Ikiwa “injili” ambayo umefundishwa kuifuata imekuwa ikikuvuta kuifuata njia ya dini na kujihesabia haki-kibinafsi, basi ni dhahiri kuwa huelewi ukweli wenye utukufu kwamba Kristo ameweza kukufanya uwe huru kwa injili yake.

Kama Biblia yako bado imekuwa ni msitu mnene, na imekuwa ni kitabu kilichofungwa kwa uelewa wako, basi macho yako bado hayajaangaziwa kuelewa wa kile ambacho Mungu amekifunua katika ile SIRI ya Kristo.

Kuna hisia/mihemko siku hizi za kufanya miujiza ya uponyaji ili kuwafanya watu vipofu wa macho ya nyama waone. Lakini hata hivyo, ‘mponyaji’ mwenye uono wa 20/20 hawezi kuona SIRI ya Kristo.

Kuna faida gani ya kuwafanya vipofu waone, wakati wote wawili (mponyaji na mponywaji) hawajui SIRI ya Kristo?

Ni kwa kuhubiriwa kwake ufunuo wa SIRI ya Kristo pekee ndiko ambako hufanya ‘macho’ yafunguliwe kwa sababu ya uwazi wa injili na kweli ya Biblia iliyogawanywa sawa sawa. Ni jukumu letu kuwafanya watu wote waone…

“na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote” (Waefeso 3:9)

Author: Festus Patta

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *