Home 2020 August 01 Bila Israeli, Bila Maagano, Bila Sheria

Bila Israeli, Bila Maagano, Bila Sheria

Bila Israeli, Bila Maagano, Bila Sheria

Tunao Wokovu – Bila Israeli, Bila Maagano, Bila Sheria!

Mahubiri mengi ya Biblia yanahusu wokovu. Mafundisho mengi ya Biblia pia yanasema wokovu utakuja kupitia Israeli, kama ilivyoahidiwa katika maagano, na matendo ya sheria yakiwa ndilo hitaji kuu.

Kristo alimtuma Paulo kuutangaza wokovu kulingana na mpango wa SIRI bila Israeli, bila maagano, na bila sheria. Kwa sababu hiyo wokovu sasa unapatikana kwa Kristo Yesu peke yake.

Bila Israeli

Wakati ule Mungu alipokuwa akifanya kazi katika ulimwengu huu kwa njia ya wateule wake, wokovu ulisemwa kuwa “watoka kwa Wayahudi” (Yesu, Yohana 4:22). Wokovu kwa mataifa mengine ungekuja kutokana na kutimilika/kukamilika (kupata utukufu) kwa Israeli, na hapo ndipo tu mataifa ya dunia yangeweza kubarikiwa.

Kuwa Myahudi ilimaanisha kuwa wa kwanza kupokea baraka za Mungu, na baadae kuwa njia, yaani bomba la kupitishia baraka na wokovu kwa watu wa Mataifa (Wayunani).

Sababu ya Kristo kumtuma Paulo kwa watu wa Mataifa, ilikuwa ni kwa sababu Israeli ilikuwa imekataa vyote; walimkataa Yesu mwenyewe na wokovu wake aliokuwa amewaletea (Warumi 11:25). Ni kweli kwamba, Paulo alienda kwanza kwa Wayahudi, lakini naye hakupokelewa. Watu wa Mataifa hatahivyo, walikuwa wakiupokea wokovu bila Israeli kwa kuhubiriwa kifo na ufufuko wa Kristo.

Paulo anathibitisha kwamba, wote wawili, Myahudi na Mmataifa wako chini ya dhambi (ni watenda dhambi), na hivyo kuwa Mwisraeli leo hakuna faida ya kipekee kwenye wokovu unaopatikana kwa neema kupitia imani. Leo miaka 2000 baadaye, hali imebaki kuwa ile ile, kwamba watu wa Mataifa wanaendelea kuokolewa – kwa neema, kwa imani – wakati taifa la Israeli kwa ujumla, bado limemkataa Yesu na wokovu wake.

Wokovu, katika majira haya ya ufunuo wa ile siri, majira ya uachilio wa neema ya Mungu, unapatikana bila Israeli:

“Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi; kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja” (Warumi 3:9-12)

na tena…

“Kwa maana kama ninyi zamani mlivyomwasi Mungu, lakini sasa mmepata rehema kwa kuasi kwao; kadhalika na hao wameasi sasa, ili kwa kupata rehema kwenu wao nao wapate rehema. Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote” (Warumi 11:30-32)

Bila Maagano

Kile ambacho kiliifanya Israeli kuwa watu wateule wa Mungu kilikuwa ni maagano waliyopewa wao peke yao. Wayunani/Mataifa hawakuwa na upendeleo huo au kupata faida ya kuwa na Maagano yoyote na Mungu.

Hata wakati ikitokea Israeli walishindwa (walikengeuka/walipotoka), waliweza kuweka madai yao katika maagano ya ahadi ambayo Mungu alikuwa ameyafanya na baba zao, Daudi, na manabii. Mungu alikuwa amewaahidi kuwaokoa! Ujasiri wao (audacity) katika wokovu ulikuwa unapatikana katika maagano ambayo Mungu alikuwa ameyafanya.

Kinyume chake, Paulo anahubiri imani kamili ya wokovu kwa watu ambao hawakuwa na maagano yoyote. Je, ni kwa msingi gani ambao watu hao wanaweza kuwa na uhakika/ujasiri huo? Paulo anaeleza kuwa kazi ya wokovu ilikuwa tayari imekamilika, na ilikuwa inatolewa kwao bure kwa imani katika damu ya Yesu na sio katika maagano ya mababa…

Wakati unabii uliahidi matumaini ya baadaye ya wokovu, yaani ilikuwa ni ahadi ambayo bado haijatimizwa. Paulo, hata hivyo, alihubiri umiliki wa sasa wa wokovu sawasawa na ufunuo wa ile siri.

Mungu hana wajibu wowote wa kutimiza agano lolote kwa Kanisa, Mwili wa Kristo, kwa sababu hakuwahi kufanya agano lolote na hicho kiumbe, kinachoitwa ‘Kanisa – Mwili wa Kristo’. Wokovu hutolewa bure kwa neema kwa imani bila wajibu au mahitaji ya kutekeleza. Mungu na Israeli bado wana wajibu wa kutimiza chini ya maagano waliyoingia kabla ya wokovu kuja tena kwao:

“Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao” (Warumi 11:27)

Ni katika Siri ya Kristo pekee, ndiko wokovu huja bila agano la ahadi, bali ni kwa njia moja tu ya ahadi katika Kristo kupitia injili:

“ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache. Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili” (Waefeso 3:3-6)

Bila Sheria

Mwanadamu anawezaje kuwa mwema bila ya kuwa na utii kwa sheria au amri za Mungu? Hii imefafanuliwa vizuri sana katika waraka wa Paulo kwa Warumi 3-5.

“kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti” (Warumi 3:20-22)

Sheria ilikuwa mada (sehemu kuu) ya Agano la Kale la Israeli, na sheria hiyo ilikuwa na marekebisho katika agano jipya kwa Israeli, lakini katika maeneo yote hayo mawili sheria ya Mungu ilikuwa ndicho kuthibitisho cha haki yao na imani.

Lakini kulingana na ufunuo wa ile siri, Paulo anaongelea juu ya wokovu unaopatikana bila sheria, ambao unatolewa bure kwa watu wote waaminio.

Israeli itarejeshwa. Maagano ya Mungu yatatimizwa. Sheria ni takatifu, ya haki, na njema, na siku moja itakuwa ikihubiriwa kwa mataifa yote.

Siri ya Kristo inaathiri jinsi wokovu unavyohubiriwa. Wokovu kulingana na unabii ulikuwa ni kupitia Israeli, chini ya maagano, na uliambatana na sheria.

Siri ya Kristo ni jinsi wokovu unavyowajia wote bila Israeli, bila maagano, na bila sheria. Hii ni hekima ya siri ya Mungu katika Kristo Yesu ilikuwa imefichwa kwa Mungu tangu ulimwengu kuanza, lakini sasa imefanywa ijulikane kwa mataifa yote.

Kwa Utukufu wa Kristo Yesu

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *