Home 2020 February 11 Siri ya Wokovu

Siri ya Wokovu

Siri ya Wokovu

Tunaishi wakati maalumu katika historia ambapo wokovu unaweza kufafanuliwa. Kufafanuliwa huko hakutokani na maendeleo ya sayansi, lugha au falsafa; bali kunatokana na Mungu mwenyewe kutupa ufunuo wa ile siri ya injili, siri ya wokovu wetu.

Ayubu aliwahi kuuliza, “mtu huwaje mwenye haki mbele za Mungu?” (Ayubu 9:2). Daudi aliomba rehema na huruma ya Mungu kwa kusema hivi: “Ee Mungu, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu” (Zaburi 51:1). Kwa nini Mungu mwenye haki amrehemu na kumsamehe muuaji na mzinzi? Daudi baadaye aliandika maneno haya, “Wala usimhukumu mtumishi wako, Maana kwako hakuna aliye hai mwenye haki” (Zaburi 143:2). Lakini kwanini Mungu huyu mwenye haki asiwe na hukumu kwa wakosaji? Utetezi pekee wa Daudi ulikuwa, ‘hakuna mwenye haki mbele za Mungu’. Sulemani, pamoja na hekima aliyopewa na Mungu, hakuweza kujua kwa namna gani Mungu anaokoa. Alitambua tu ya kwamba “hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi” (Mhubiri 7:20), na jumuisho lake likawa hili, “Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndivyo impasavyo mtu” (Mhubiri 12:13). Hata hivyo, “Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe?” (Yona 3:9).

Hakuna aliyeweza kusema. Wokovu ulikuwa ni siri. Mungu alikuwa ni mwingi wa rehema, alikuwa akisamehe, alitoa wokovu, lakini hakuna aliyeweza kuelezea au kufafanua ni kwa namna gani Mungu mwenye haki aliweza kumhesabia haki mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe, ambaye hakuwa na kitu chochote chema, isipokuwa imani tu!

Watu wengi wanaotamani kuokolewa leo wanajua wokovu unahitajika na kwamba Bwana ndiye pekee awezaye kutoa, lakini watu hao ni ‘wajinga’ wa habari njema ya wokovu wetu (Waefeso 1:13).

Wokovu ulikuwa na siri, na utabakia kuwa siri mpaka hapo watu watakapotambua na kuukubali ujumbe uliofunuliwa kwa Mtume Paulo, kiongozi wa watenda dhambi (1 Timetheo 1:15-16).

Wokovu ilikuwa ni sehemu ya kusudi la Mungu lililofichwa tangu mwanzo, hekima iliyofichwa tangu kabla ya ulimwengu kuwako, ambayo ilifunuliwa kwa Mtume Paulo ili aifundishe na kuihubiri siri hiyo kwa wote, ulimwenguni kote (2 Timetheo 1:9-11).

Ukisoma 2 Timetheo 3:15 neno la Mungu linasema maandiko matakatifu yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu, lakini bado hatuoni wokovu ukieleweka kwa watu katika historia ya maandiko. Ilikuwa ni mpaka pale tu maandiko ya mwisho yalipoandikwa na mtume kwa watu wa Mataifa, Mtume Paulo, ndipo tunaweza kuelezea hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi katika kuleta wokovu kwa wote (Waefeso 3:9-11).

Wokovu ulikuwa ni siri. Siri hiyo sasa imefunuliwa. Swali lilikuwa ni kwa namna gani Mungu anaweza kuwahesabia haki wenye dhambi?

“Wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu (Warumi 3:24-26).

Sasa inafahamika ya kwamba ni kwa neema ya Mungu kupitia kwa Bwana Yesu Kristo kwao wote wamwaminio:

“Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa” (Tito 2:11)

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *