Home 2020 February 11 Neema ya Mungu (ii)

Neema ya Mungu (ii)

Neema ya Mungu (ii)

Kuwepo kwa Neema ya Mungu ni habari njema kwetu. Habari njema hii inaleta furaha kuu kwamba Mungu hayuko kinyume chetu bali yupo kwa ajili yetu, yuko pamoja nasi katika Kristo, yupo ndani yetu. Je, liko jambo lolote unalodhani linaweza kututenga na upendo huo wa Mungu? Paulo anasema halipo, halijawahi kutokea; na kamwe halitokuwepo! “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho cho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Warumi 8:38-39).

Unajua ni kwa nini Paulo ana ujasiri wa kutupa uhakikisho huo? Ni kwa sababu anajua, hakuna jambo lililokuwa kubwa na ngumu kwa Mungu kama kumtoa (kumwua) mwanae pekee kipenzi aliyempenda kuliko vyote, Yesu Kristo; na Mungu alifanya hivyo kwa ajiri yetu, wewe na mimi! Ndio maana Paulo anatuuliza lipo jambo gani ngumu lingine lililobakia ambalo Mungu atashindwa kulifanya zaidi ya lile la kumtoa Kristo Yesu? Hakika halipo! “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, ATAKOSAJE kutukirimia na mambo yote pamoja naye? (Warumi 8:32). Ukilijua hili ‘Ukristo’ utakuwa na maana kwako, wala hautahangaika kufanya au kujitahidi kuyatimiza yale ambayo Mungu alishayatimiza kwa ajili yako; kwa sababu yake yeye mwenyewe!

Neema ya Mungu, zaidi ya maelezo yo yote yale, ni bora zaidi kuliko ‘mkusanyiko’ wa dini zote za ulimwengu huu ukiziweka pamoja, ukiwemo na ‘Ukristo’. Dini zinasema ni lazima uwe ‘msafi’ (kwa viwango vyao) kabla hujaweza kumkaribia Mungu, lakini NEEMA inasema ‘njoo kama hivyo ulivyo!’ Kama ilivyo kwa mvuvi wa samaki, ambaye anamvua samaki na magamba yake, na uchafu wake wote, vile alivyo; na baada ya kumvua humtengeneza samaki huyo yeye mwenyewe kwa kadri anavyotaka kumtumia, pamoja na kumtia viungo; Mungu pia, ndivyo afanyavyo kwa sababu ya pendo lake: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mathayo 11:28).

Juhudi za wanadamu kumtafuta Mungu (dini), zinahitaji ufanye hili na lile ili ukubarike na Mungu, lakini neema ya Mungu inasisitiza Kristo Yesu alifanya yote, aliyakamilisha yote, wala hayahitaji nyongeza kutoka kwako! Dini zinasema ni lazima utunze sheria na kutoa dhabihu tena zinazouma, lakini neema ya Mungu inatangaza kuwa Kristo amezitunza na kuzitimiza sheria zote kwa niaba yetu na dhabihu aliyoitoa haina mbadala wake. Iko shida hapa, kwa sababu yale ambayo neema ya Mungu inayasisitiza yako kinyume na yale ambayo dini inayasisitiza; lakini ole wake mtu yule anayeidharau neema ya Mungu: “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika NEEMA ya Kristo, na kuigeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe” (Wagalatia 1:6-8).

Tunaona katika maandiko matakatifu ya kwamba upendo na neema ya Mungu ni zaidi sana, na iliyopindukia, na iliyopita kiasi, katika uwingi na ubora; kwa ujumla wake, upendo na neema ya Mungu havielezeki kwa kipimo chochote kile wala maelezo yoyote yale ya kibinadamu kwa sababu vimepanuka sana na kuvuka upeo wa uelewa wetu. Kile unachofikiri, pale (wakati) unapoutafakari upendo wa Mungu kwako; hakika ni ‘duni’ sana kwa uhalisia wake ukilinganisha na pendo halisi la Mungu lisiloelezeka kwako. Hivyo tunaweza kusema kuwa neema ya Mungu ni kile tunachodhania upendo wa Mungu unafanana nacho, lakini neema iliyopindukia, iliyozidi sana, ndiyo hasa upendo wa Mungu ulivyo.

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *