Home 2024 April 03 PALIKUWA NA MTU KAISARIA!

PALIKUWA NA MTU KAISARIA!

PALIKUWA NA MTU KAISARIA!

Katika kuyarejea Maandiko Matakatifu, katika harakati zangu za kuandaa ‘nyumbe’ mbalimbali kwa ajili ya makala kama hizi na mafundisho mengine Kanisani, nilifungua Biblia yangu kukiendea kifungu ninachokipenda zaidi (kwa sababu maalumu) katika kitabu cha Matendo ya Mitume, Sura ya 10.

Katika huduma yangu kwa Mwili wa Kristo, nimekuwa nikihubiri na kufundisha mara nyingi kupitia Kitabu cha Matendo, kwa hiyo, habari ya Kornelio; akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, ni habari iliyo wazi zaidi katika kumbukumbu zangu.

Lakini, wakati nataka kuirejea tena habari hiyo safari hii, kabla sijaingia ndani kwenye kiini cha maandiko hayo, maneno manne ya kwanza ya Sura hiyo ya 10, yalionekana kwa mwonekano mkubwa zaidi na kuyavutia hapo macho yangu na hisia zangu hapo na kunitoa kutoka kule ambako nilitaka kueleka. Ilikuwa ni kana kwamba, yaliandikwa kwa maandishi mazito na herufi kubwa, kwamba: “PALIKUWA NA MTU KAISARIA

Roho yangu ilifurika ghafla kwa utambuzi wa kiwango cha upendo wa Mungu kwa mwanadamu, na ubinafsi wake (kwa mtu mmoja mmoja). Bila shaka, kulikuwa na watu wengi walioishi duniani wakati wa Kornelio, lakini Mungu alipendezwa na huyu mtu MMOJA. Nina hakika pia kwamba, kulikuwa na mambo mengi ambayo yangeweza kuteka fikira za Mungu wakati huo, lakini Yeye alipendezwa na huyu PEKEE!

Ilinifanya nifikiri kuwa, pamoja na mambo yote yanayoendelea ulimwenguni humu leo, yanayotufanya tukose kuona jambo lile lililo muhimu kwetu – lakini Mungu, kamwe, hafanyi hivyo. Yeye, anapendezwa na maisha yetu binafsi na anatamani kujihusisha nayo. Hakika, Mungu wetu ni mkuu sana, kwamba pamoja na majaribu na misukosuko yote tunayopitia maishani mwetu, bado tunaweza kumwomba na Yeye akasikia maombi yetu. Na sio kusikia tu, bali Yeye kuhusika nayo kibinafsi kwa ajili ya ustawi wetu.

Unaweza kufikiri kwamba Matendo 10, ni ‘hadithi’ tu ya jinsi Mungu alivyomtumia Kornelio kuelezea kuvunjika kwa ukuta wa kati wa utengano wa mwili, na mpito kutoka kwa mpango wa ufalme wa Mungu hadi mpango Wake wa neema; Ingawa hiyo ni kweli, lakini pia, ‘hadithi’ hii inaonyesha jinsi Mungu anavyojali watu binafsi (mtu mmoja mmoja), kwa kuwa Yeye anataka watu wake wote waokolewe…!

Lakini huo sio mwisho wa kuhusika Kwake; Mungu pia anataka watu wake wote wafikie ujuzi wa kweli (1 Timotheo 2:4). Kwa kadiri tunavyoweza kujua ukweli mwingi kumhusu Yeye, ndivyo tunavyoweza kumwamini kwa ukamilifu wake. Mungu pia, anataka uhusiano wa kibinafsi, na wa karibu na wewe, na mimi; Kwa sababu Mungu, anatupenda na anatujali kwa mahitaji yetu yote.

Ndiyo kusema, wakati majaribu ya maisha yanapokushusha chini na kuonekana kwamba tumaini lote limetoweka, kumbuka: wewe ni MTU FULANI – mwanaume au mwanamke, na Mungu anakujali.

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *