Home 2024 March 14 MTUME WA WASIO WAYAHUDI!

MTUME WA WASIO WAYAHUDI!

MTUME WA WASIO WAYAHUDI!

Si Mathayo, Marko, au Luka; wala Petro, Yakobo, au Yohana, bali Paulo peke yake ndiye aliyeandika kwenye Warumi 11:13, kwa uongozi wa kimungu, maneno haya:

“LAKINI NASEMA NA NINYI, MLIO WATU WA MATAIFA. BASI, KWA KADIRI NILIVYO MTUME WA WATU WA MATAIFA (WATU WASIO WAYAHUDI), NAITUKUZA HUDUMA ILIYO YANGU” (WARUMI 11:13)

Angalia vyema kile ambacho Mtume Paulo anachosema; kwamba yeye hakujitukuza mwenyewe, bali cheo chake, ambacho alikuwa ameteuliwa nacho na Bwana Mwenyewe akiwa katika utukufu wake.

Katika kutetea utume wake mbele ya Wagalatia, Paulo aliandika:

“KWA MAANA, NDUGU ZANGU, INJILI HIYO NILIYOWAHUBIRI, NAWAJULISHA YA KUWA SIYO YA NAMNA YA KIBINADAMU. KWA KUWA SIKUIPOKEA KWA MWANADAMU WALA SIKUFUNDISHWA NA MWANADAMU, BALI KWA UFUNUO WA YESU KRISTO” (WAGALATIA 1:11-12)

Katika vifungu vingine vingi, Mtume Paulo amejitokeza na kuzungumza kama mwakilishi mwenye usemi wa moja kwa moja wa Kristo (Angalia, kwa mfano katika vifungu hivi: 1 Wakorintho 11:23; 15:3; Waefeso 3:1-3; 1 Wathesalonike 4:15; n.k.)!

“Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate”

“Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko”

“Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa; ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache”

“Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti”

Kwa Timotheo, Mtume Paulo aliandika hivi kuhusu maandishi yake yeye mwenyewe: “Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa, amejivuna; wala hafahamu neno lo lote” (1 Timotheo 6:3-4a). Hili kimsingi, linaonyesha kwa mkazo unaostahili dai la Mtume Paulo kwamba maneno yake yalikuwa ni “maneno ya Bwana Yesu Kristo“, yaliyopokelewa kutoka Kwake kwa ufunuo wa moja kwa moja.

Kwa Wakorintho, ambao walitilia shaka hili, Mtume Paulo aliandika:

“…NIKIJA, SITAHURUMIA; KWA KUWA MNATAFUTA DALILI YA KRISTO, ASEMAYE NDANI YANGU…” (2 WAKORINTHO 13:2-3).

Ushahidi wa dai hili?

Hili lilikuwa jambo kubwa lenye kuwafikirisha, kwa maana Mtume Paulo ni mtume aliyetumiwa zaidi ya mtume mwingine yeyote yule katika kueneza Injili ya Kristo na kuanzisha makanisa na katika kuwaongoza watu katika ujuvi na furaha ya wokovu. Kwa waamini wa Korintho, aliandika kile ambacho angeweza kuwaandikia maelfu mengi ya watu wengine wa mataifa leo: “Ninyi ndinyi muhuri ya utume wangu katika Bwana” (1 Wakorintho 9:2).

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *