Home 2024 March 04 TUNAHESABIWA HAKI BURE!

TUNAHESABIWA HAKI BURE!

TUNAHESABIWA HAKI BURE!

“Wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu” (Warumi 3:24)

Ni jambo lisilojulikana na wengi kwamba sisi wenye dhambi hatuhesabiwi haki kwa sababu ya kuomba kwetu, au kulipa gharama kwetu sitahiki, au kukiri uovu wetu, au kuugua kwingi mioyoni mwetu, au kulia mpaka machozi ya damu yatutoke, au kwa kufanya kitu fulani. BALI, Tunahesabiwa haki bure, kwa neema ya Mungu!

Lakini kifungu hiki cha Warumi, kitakuwa na maana zaidi kwetu, tukijifunza jinsi neno lililotafsiriwa “BURE” hapa linavyotafsiriwa mahali pengine katika Biblia. Usemi huohuo unapatikana pia katika Yohana 15:25, ambapo Bwana wetu Yesu Kristo, akinukuu kutoka Zaburi, alisema: “Walinichukia bure.”

Kwa nini wanadamu walimchukia? Yeye alikuwa akizunguka, huku na kule, bila kufanya jambo lolote baya, isipokuwa mema: Alikuwa akiwaponya wagonjwa, akiwapa vipofu kuona tena, akiwafanya viwete kurukaruka kwa furaha, akiwahubiria maskini habari njema na kuwakomboa wale wote waliokuwa wamefungwa. Hapakuwa na sababu yoyote nzuri kwao ya kupiga makelele, “Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe!” Walimchukia bure, “bila sababu.”

Lakini kwa njia iyo hiyo tunaweza kuuliza: “Kwa nini afe kwa ajili ya wenye dhambi? Kwa nini alipe dhambi zao? Hakuwa amefanya kosa lolote.” Ah, ilikuwa ni katika pendo lake lisilo na ukomo, kwamba alijitoa kwa makusudi mikononi mwa watu wenye dhambi, ili Yeye, asiye na dhambi, alipe dhambi zao.

Hakufa kifo chake mwenyewe, kwa maana kifo ni “mshahara wa dhambi.” Alikufa kifo chetu, akilipia dhambi zetu. Kwa hivyo, kama vile wanadamu walivyomchukia “bila sababu” (isipokuwa hali yao ya dhambi), vivyo hivyo Kristo “amewahesabia haki” waamini “bila sababu” (isipokuwa upendo wake Yeye mwenyewe; Upendo wa kimungu).

Na ndivyo ilivyo kwamba sasa tunaweza kutangaza habari tukufu ambayo Mungu ametutuma kuwaambia wanadamu wote, kwamba haki yake imetolewa “juu ya wale wote waaminio,” na kwamba waamini hao “wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu.”

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *