Home 2024 February 18 NENO LA KUAMINIWA

NENO LA KUAMINIWA

NENO LA KUAMINIWA

“Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi” (1 Timotheo 1:15)

Kati ya “maneno yote ya kuaminiwa” ya Mtume Paulo, hili pengine linaweza kuwa ndilo la kustaajabisha zaidi, na ambalo kupitia kwalo, watu wengi wamepata furaha ya dhambi zao kusamehewa!

Mada ni kwamba “Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi.” Lakini je, ni kwa nini hasa, Kristo alilazimika kuuacha utukufu Wake mbinguni, kama yasemavyo Maandiko, na kuja duniani katika umbo la kibinadamu ili kutuwakilisha katika malipo ya dhambi zetu? Na, ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba, kwa hakika Yeye alilipa gharama kamili kwa ajili ya dhambi za watu wote; kwa kuwa hakuwa mtu tu wa kawaida Yeye huyo aliyekufa pale msalabani Kalvari.

Malipo Yake hayo, yalikuwa ni kamilifu sana, kiasi kwamba Mtume Paulo hakuweza kujizuia kusema kwa kustaajabu kwamba, Yesu Kristo; “Alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi, ambao mimi ni mkuu wao.” Mtume Paulo, mwenyewe, ambaye ingawa wakati fulani alikuwa ni adui mkuu wa Kristo hapa duniani, sasa alikuwa ameokolewa Naye na alikuwa amefikia kujua furaha ya dhambi zake kusamehewa…

Janga kuu ni kwamba, watu wengi hawaoni hali yao ya kutokuwa na tumaini la kusamehewa dhambi zao mbali na Kristo. Bado, ndugu hao, hawajaona jinsi wanavyopungukiwa na utukufu na utakatifu wa Mungu. Wote wanajua, kuwa wao ni watenda-dhambi, lakini bado hawaoni kwamba hali yao hiyo haina tumaini lolote na kwamba wanahitaji Mwokozi. Kwa sababu hiyo, ndugu hawa wanaendelea kujaribu, na kujaribu, na kujaribu – na ushahidi walionao katika mioyo yao ni kwamba, wanaendelea kushindwa, an kushindwa, na kushindwa; kujiokoa wenyewe!!!

Ni hekima iliyoje kwetu, kuziungama dhambi zetu mbele za Mungu, na kuchukua nafasi yetu ya wenye dhambi, ili Yeye aweze kutuokoa? Hii ni hatua ya kwanza na ya muhimu katika safari yetu ya kuelekea mbinguni. Tunapofanya hivi, tunajiweka katika nafasi ya kukubali toleo la Mungu la msamaha kamili wa dhambi zetu na kuhesabiwa haki kupitia kwa Kristo Yesu, ambaye alikufa ili kulipa adhabu la dhambi zetu.

Kwa kuwa, hakuna hata mmoja wetu aliye mkamilifu na kwamba sisi sote tumefanya dhambi, “hili,” kwa “kweli,” ni “neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi.”

Je! Ni kwa nini sasa, usiliamini NENO LA MUNGU, na ukamkubali KRISTO YESU kama Mwokozi wako na uokoke leo???

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *