Home 2023 November 12 MUNGU ASIYEWEZA KUSEMA UONGO ALIAHIDI!

MUNGU ASIYEWEZA KUSEMA UONGO ALIAHIDI!

MUNGU ASIYEWEZA KUSEMA UONGO ALIAHIDI!

“Katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele” (Tito 1:2)

Katika Bahari ya Mediterania kuna kisiwa ambacho katika siku za Mtume Paulo kilikuwa na sifa mbaya sana; Jina lake ni Krete. Kwa Tito, mchungaji aliyeachwa ili ‘ayatengeneze yaliyopunguka’ miongoni mwa wakazi wa huko, Mtume Paulo aliandika hivi: “Mtu wa kwao, nabii wao wenyewe, amesema Wakrete ni waongo siku zote…” (Tito 1:12), na akaongeza kusema: “Ushuhuda huu ni kweli” (Mstari wa 13).

Mtume Paulo alijua jambo hili kuwa ni ukweli usiopingika, kwa kuwa alikuwa amejitaabisha kwa kufanya kazi kati yao. Kwa hakika, hata historia ya kilimwengu inashuhudia sifa hiyo ya Wakreti, kwa maana tunaambiwa kwamba katika nyakati za kale kumwita mtu Mkreti kulikuwa ni sawa na kumwita mtu huyo kuwa ni ‘mwongo’!

Ni jambo la kushangaza kuona kuwa katika mazingira hayo Mtume Paulo alikuwa amefaulu kuanzisha makusanyiko machache madogo madogo ya Kikristo kwenye kisiwa hiki na kwamba Tito sasa alikuwa akifanya kazi huko akiwa mrithi wake! Lakini pia, ni jambo lenye kutia moyo sana kwa Tito na waamini hao wachache, wakiwa wamezungukwa kila upande na watu hawa waongo; wasiotii; wenye maneno yasiyo maana; wadanganyaji; na wasioweza kutegemewa, kwamba Mtume Paulo angeweza kuandika juu ya “uzima wa milele, ambao Mungu, asiyeweza kusema uwongo, aliahidi”!

“Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? (Hesabu 23:19)

Tunamshukuru Mungu, mamilioni wameamini Neno Lake leo, hasa kuhusu wokovu kupitia kazi ya ukombozi inayotosheleza na iliyokamilika iliyofanywa na Kristo Yesu pale msalabani Kalvari, na hao waliomwamini wametambua kuwa hiyo ni kweli yenye baraka.

Katika vifungu vingi vya Maandiko Mungu ameahidi uzima wa milele kwa wale wanaomtumaini Kristo na malipo yake kwa ajili ya dhambi zetu:

“Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu” (1 Wakorintho 15:3)

“Ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki” (Warumi 4:25)

“Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele” (Yohana 3:36)

“Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka” (Matendo 16:31)

Mchukue Mungu katika Neno Lake; Ahadi zake ni kweli na ni amini; kwa kuwa “MUNGU, ASIYEWEZA KUSEMA UONGO, ALIAHIDI.”

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *