Home 2023 November 05 Enenda Zako Wala Usitende Dhambi Tena!

Enenda Zako Wala Usitende Dhambi Tena!

Enenda Zako Wala Usitende Dhambi Tena!

Waandishi na Mafarisayo waliojiona kuwa ni wenye haki (waadilifu) nao walikuwa wamemleta mwanamke aliyeanguka uzinzini kwa Yesu na, “walipomweka katikati,” wakaanza kumshitaki kwake, wakisema “mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe unasemaje?” (Yohana 8:4-5).

Waandishi na Mafarisayo hao walikuwa wakimtumia mwanamke huyu aliyeanguka dhambini ili kumweka ‘kitanzini’ Bwana kukubali kwamba mwanamke huyu apigwe mawe, na asingefanya hivyo angekuwa amejiweka dhahiri (amejianika) kwa shtaka la kukana (kupinga) Sheria ya Musa.

Mara ya kwanza Yesu alijifanya “kana kwamba hakuwasikia”, lakini, walipozidi kumhoji, walikipata walichokuwa wakikitafuta! Bila kutumia nguvu, kwa upole akawaambia: “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe”; Bwana akainama tena chini ili kuiacha hukumu hiyo ifanye kazi yake! Kabla ya hapa, ndugu wale walikuwa “wamemweka katikati” yule mwanamke; Lakini sasa kibao kiliwageukia, Bwana alikuwa “amewaweka wao katikati” na, “wakiwa wamehukumiwa na dhamiri zao wenyewe”, “wakatoka mmoja baada ya mwingine; … akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati” (Msitari wa 9).

Na hapo alisimama mwanamke peke yake mbele Yake: mwenye dhambi mkuu mbele ya Mwokozi mkuu! Kwa kuwa hakuna Mwandishi wala Farisayo hata mmoja aliyethubutu kumtupia jiwe, Bwana alisema: “Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena” (Msitari 11).

Hivyo ndivyo Bwana alivyomsamehe kwa neema mwanamke huyu mdhambi, lakini bila kupuuza matakwa ya Sheria. Yesu hakuwa amekana kwamba mwanamke huyo alistahili adhabu; lakini aliwakumbusha Waandishi na Mafarisayo kwamba nao walikuwa ni wenye dhambi; na kwamba wao (Waandishi na Mafarisayo), kama ilivyokuwa kwa yule mwanamke, nao pia walihitaji Mwokozi.

Hakika, Mungu ni wa kutukuzwa daima! Kwa kuwa “Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu”, Mungu sasa anaweza kutusamehe kwa haki – na kwa HAKIKA Yeye atatusamehe, IKIWA tu tunakiri dhambi zetu na kuonyesha hitaji letu la Mwokozi, na tusijiunge na kundi la wale wanaojiona kuwa wenye haki kwa matendo yao ambao wanaendelea “kuithibitisha haki yao wenyewe na kuikana haki ya Mungu” (Warumi 10:3).

“Neno hili ni la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa WENYE DHAMBI…” (1 Timotheo 1:15). Mungu ni mwenye neema nyingi kwa wale ambao watakiri dhambi zao na hitaji lao la Mwokozi:

Kwa maana yeye yule ni Bwana wa wote, NI MTAJI KWA WOTE WAMWITAO; KWA KUWA, KILA ATAKAYELIITIA JINA LA BWANA ATAOKOKA” (Warumi 10:12,13).

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *