Home 2023 October 15 HAKI YA MUNGU

HAKI YA MUNGU

HAKI YA MUNGU

Kuna maneno mengi ya kitheolojia ambayo, watu wengi, hasa wale wanaojiita Wakristo; ambao ni wengi – hawayaelewi. Miongoni mwao ni neno la Kibiblia “haki”. Kwa kweli, ingawa, neno hili ni rahisi sana na tunapaswa kuelewa vyema kuhusu haki ya Mungu hata kabla ya kujifunza juu ya upendo Wake.

Tunaposema kwamba Mungu ni mwenye haki, tunamaanisha tu kwamba kile anachofanya kiko sawa wakati wote; kwamba hatafanya na hawezi kufanya chochote kile ambacho hakiko sahihi. Hii ndiyo sababu Mtume Paulo anatangaza katika Warumi 1:16,17 kuwa:

“Siionei haya Injili; kwa maana ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye; KWA MAANA HAKI YA MUNGU IMEFUNULIWA (INADHIHIRISHWA) NDANI YAKE”

Tunajivunia kutangaza injili ya neema ya Mungu kwa sababu injili hiyo inasisitiza juu ya haki ya Mungu. Injili hiyo haituambii kwamba Mungu atapuuza dhambi zetu au kuzifumbia macho au kuzifanyia mizaha na kutusafirisha kwa ‘magendo’ kwenda mbinguni. Injili hiyo pia haituambii kwamba atatusamehe tu ikiwa tutajuta vya kutosha au kufanya matendo mema ya kutosha ili ‘kusawazisha’ dhambi zetu. La hasha!

Injili ya neema ya Mungu” inategemea (imejengeka juu ya) haki yake yeye Mungu pekee. Ni ujumbe wenye uzuri wa kipekee kwamba “Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu”, na kwamba yeye alilipa malipo kamili ya dhambi hizo ili aweze kutupa msamaha kwa haki na kututangaza kuwa sisi ni wenye haki.

Warumi 3:26 inalibainisha hili kwa uzuri. Katika andiko hilo, Mtume Paulo anatangaza kwamba kwa vile dhambi zetu zote (zilizotangulia, za sasa na zijazo) zililipiwa na Kristo pale Kalvari, Mungu sasa anaweza “kuwa mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu”.

Kwa karne nyingi sasa, watu wa dini, wamekuwa wakiambiana wao kwa wao kuwa: “Ni lazima tujute dhambi zetu kikamilifu (kweli kweli) na tufanye mema yote tuwezayo na hakika ndipo Mungu atatusamehe na kutukubali”. Lakini hiyo sio injili! Injili inatupa msingi thabiti zaidi wa kusimika miguu yetu juu yake. Injili inasema kwa kila mwanamume, kila mwanamke, kila mtoto na kila mwanadamu: “Dhambi zako ZIMELIPWA na Kristo pale Kalvari; Mtumaini Yeye na utaokoka”.

Hii kwa hakika, ndiyo injili [habari njema], kwa kuwa inategemea malipo ya haki ya adhabu ya dhambi.

Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *