Home 2023 August 21 UTOAJI KATIKA AGANO JIPYA

UTOAJI KATIKA AGANO JIPYA

UTOAJI KATIKA AGANO JIPYA

Agano Jipya lina uwajibikaji mkubwa wa kifedha kuliko zaka, lakini umejengeka katika dhana tofauti kabisa. Zaka kamwe haitajwi kama agizo kwa waumini wa Agano Jipya – si kama sheria, kanuni, au hiari ya mazoea. Mitume waliwahimiza sana waumini watoe fedha, lakini mahimizo yao hayakuwa kwa namna yoyote ile yakihusiana na zaka. Walipowaagiza waumini kuwasaidia maskini na wajane na yatima na kusaidia wahudumu wa injili, katu-katu hawakunukuu maandiko kuhusu zaka; hawakuwahi kuikumbuka Malaki 3:10!

Mtume Paulo aliandika zaidi juu ya suala la utoaji wa kifedha kuliko waandishi wengine wote wa Nyaraka za Agano Jipya. Alipowaelekeza waumini kuhusu wajibu wao wa kutoa fedha alinukuu maandiko ya Agano la Kale ili kusaidia mafundisho yake, lakini siyo lile ‘maarufu’ la kutoa zaka; Hakuwahi kufanya hivyo! Ndiyo kusema, hakuna msingi wowote wa kusema kwamba kanisa la Agano Jipya lilizingatia fundisho la zaka kuwa kielelezo cha utumishi wa kifedha. Hakuna ushahidi wa kimaandiko pia wa kusema kwamba mitume waliichukulia zaka kuwa ni kanuni ya milele kwa nyakati zote au kwamba ndio ufunguo wa baraka za kifedha kwa Wakristo.

Katika 1 Wakorintho 9, Mtume Paulo anatoa mafundisho ya kina juu ya kwa nini wahudumu wa injili wana haki ya kuungwa mkono kifedha na kwa nini mwili wa Kristo una wajibu wa kufanya hivyo. Mtume Paulo amerejea hoja kadha wa kadha za kitheolojia ili kuthibitisha kile alichokuwa akikifundisha. Kama zaka ingekuwa inahitajika katika hilo, hii ingekuwa ndiyo fursa nzuri kwake kunukuu aya za kutoa zaka kama mamlaka ya kimaandiko kwa kile anachokisema; lakini hafanyi hivyo, ASILANI!

Katika 1 Wakorintho 9:7 Mtume Paulo anaanza mafundisho yake kwa kurejea matumizi ya akili ya kawaida (common sense):

“Ni askari gani aendaye vitani wakati wo wote kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi, asiyekunywa katika maziwa ya kundi?”

Katika mstari wa tisa anairejea Sheria ya Musa inayosema: “Usimfunge kinywa ng’ombe apurapo nafaka.” (Kumbukumbu 25:4).

Katika mstari wa kumi na tatu wa 1 Wakorintho 9, Paulo anarejelea kanuni ya Agano la Kale kwamba wale wanaohudumu katika hekalu na madhabahuni wametawazwa kushiriki (kutumia) vitu vinavyoletwa kama dhabihu na matoleo. Katika mstari wa kumi na nne ananukuu maneno ya Yesu:

“Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili.”

Hii ni rejea ya kile Yesu alichowaambia wanafunzi wake wakati alipowatuma. Katika Mathayo 10:10 tunasoma maneno yake haya, “maana mtenda kazi astahili posho lake,” na katika Luka 10:7, “maana mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake.”

Katika 1 Timotheo 5, Paulo anawafundisha waumini kuwaunga mkono wahudumu wa injili. Hapa tena, ananukuu Kumbukumbu la Torati 25:4 na maneno ya Yesu, lakini hasemi chochote kuhusu zaka!

“Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha. Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng’ombe apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake.” (1 Timotheo 5:17-18)

Yesu pia alisema mambo mengi juu ya suala la utoaji ambayo hayakutegemea au kuihusu zaka. Utafiti wa kina na huru wa mawaidha au mafundisho yote ya Agano Jipya yanayohusu utoaji wa kifedha yanaonyesha mtazamo tofauti kabisa kuliko ule unaohubiriwa mara nyingi na watu wengi leo. Yesu mwenyewe ndiye kielelezo cha juu kabisa cha motisha na kusudi lolote la utoaji. Alitoa kwa sababu alikuwa na moyo wa upendo (alipenda kutoa) na alitoa ili kubariki.

Kanisa halihitaji zaka ili kufadhili kazi ya Mungu hapa duniani. Utoaji katika Agano Jipya umejengeka katika ‘mchakato’ ulio bora zaidi. Mkristo mwamini (aliyezaliwa mara ya pili) ni mmoja pamoja na Kristo na anamilikiwa naye. Maana ya asili yake mpya ni kuishi kwa ajili ya Kristo pamoja na mali zake zote, moyo wake wote, akili zake zote, roho yake yote, nguvu zake zote, na pesa zake zote.

Orodha ifuatayo inajumuisha baadhi ya mafundisho, mawaidha au mitazamo ya kimaandiko kuhusiana na utoaji katika Agano Jipya. Haya yanaweza kutumika kama msingi wa utoaji wa kifedha kanisani leo. Mengi ya haya, mara nyingi, hupuuzwa kwa sababu ya kujishughulisha na kutumia kanuni ya Agano la Kale ya kutoa zaka ili kuhamasisha watu katika utoaji wao.

  • Kumpa Mungu utukufu (Mathayo 5:16; 2 Wakorintho 9:13).
  • Kueleza asili ya Mungu (Mathayo 5:42, 45; Luka 6:35; 2 Wakorintho 9:9).
  • Umepokea bure (Mathayo 10:8; 2 Wakorintho 9:15).
  • Mfanya kazi anastahili ujira wake (Mathayo 10:10; Luka 10:7; 1 Wakorintho 9:4-14; 2 Wakorintho 11:8).
  • Ni jukumu la kifamilia (Mathayo 15:3-6; Marko 7:9-13; 1 Timotheo 5:8-16).
  • Kuonyesha huruma (Mathayo 15:32, 18:27; Marko 8:2).
  • Kuwa na hazina mbinguni (Mathayo 19:21; Marko 10:21; Luka 12:33, 14:12-14, 18:22).
  • Fanyeni kama kwa Bwana (Mathayo 25:40,45; Luka 8:3, 19:31; Wakolosai 3:23).
  • Kufuata mfano wa Yesu (Marko 8:34-35; Luka 9:23-24; Waefeso 5:2).
  • Kumtii Bwana (Luka 6:30; 2 Wakorintho 9:12-13).
  • Mtapewa (Luka 6:38; 2 Wakorintho 9:6-13; Wagalatia 6:7-9; Waefeso 6:8; Wafilipi 4:10-19).
  • Kuweka moyo safi (Luka 11:41; 1 Timotheo 6:10).
  • Kuwa msimamizi mzuri (Mathayo 25:14-30; Luka 12:42-48, 16:9-13, 19:12-26; 1 Wakorintho 4:2; 1 Petro 4:9-10).
  • Kukuza ufalme wa Mungu (Luka 18:29; Wafilipi 1:3-5; 2 Wakorintho 8:1-5, 11:7-9).
  • Kuonyesha upendo kwa ndugu na watu wote (Matendo 11:29; 2 Wakorintho 8:8, 24; 1 Yohana 3:16-18, 4:11; 3 Yohana 1:5-6, 5-6).
  • Kusaidia wanyonge (Matendo 20:35; Wagalatia 6:2; 1 Timotheo 5:16; Yakobo 1:27, 2:15-16).
  • Ni heri kutoa kuliko kupokea (Matendo 20:35).
  • Ni wajibu kwa wale wanaokuhudumia (Warumi 15:25-27; 1 Wakorintho 9:11; Wagalatia 6:6; 1 Timotheo 5:17-18; 2 Timotheo 2:6).
  • Ni mwitikio kwa neema ya Mungu (1 Wakorintho 16:1-3; 2 Wakorintho 8:1-9).
  • Kuhudumia viungo vingine vya mwili (2 Wakorintho 8:4, 9:1; Wagalatia 6:10; Waefeso 4:28).
  • Kwa urejeshaji wa siku zijazo (2 Wakorintho 8:14-15).
  • Unavyokusudia moyoni mwako (2 Wakorintho 9:7).
  • Ni kazi nzuri ambayo tuliumbwa kwa ajili yake (Waefeso 2:10; 1 Timotheo 6:17-18; Tito 3:8, 14; Waebrania 13:16; Yakobo 2:14-26).
  • Kuzaa matunda (Yohana 15:1-16; Warumi 15:28; Wafilipi 4:17; Wakolosai 1:10).
  • Kuweka tumaini letu kwa Mungu (Marko 10:23-25; Wafilipi 4:19; 1 Timotheo 6:17).
  • Kuingia katika uzima wa kweli (1 Timotheo 6:19).

Author: Festus Patta

6 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *