Home 2023 August 05 BWANA ALIPONYAMAZA!

BWANA ALIPONYAMAZA!

BWANA ALIPONYAMAZA!

Katika masimulizi mbalimbali ya huduma ya Bwana wetu Yesu Kristo hapa duniani tunazipata nyakati tatu ambapo alikataa kuwajibu chochote wale waliomwomba kitu au kumuuliza swali.

Kwanza kuna mwanamke wa Mataifa wa Mathayo 15:21-28. Binti yake alikuwa amepagawa na pepo na katika shida yake hiyo alimwomba Bwana amsaidie, “lakini Yeye hakumjibu neno lolote.” Hatimaye, katika neema Yake alimsaidia, lakini ni mpaka pale alipomfundisha somo kwamba kama Mmataifa hakuwa na madai yoyote juu Yake. Kama vile Warumi 1:28 inavyotuambia, Watu wa Mataifa walikuwa ‘wameachwa’ kwa sababu “hawakutaka kuwa na Mungu katika fahamu zao.” Katika kuhusiana na hili sisi Mataifa tunapaswa kusoma kwa makini Waefeso 2:11-12 ili tuone jinsi tulivyokuwa hatuna tumaini kabisa mbali na neema ya Mungu.

Kisha kulikuwa na mwanamke Myahudi, katika shida ya aina tofauti. Yeye alikuwa amenaswa katika uzinzi na aliletwa kwake kwa ajili ya hukumu (Yohana 8:1-11). Tofauti na mwanamke yule wa Mataifa, yeye alikuwa wa jamii iliyochaguliwa na alikuwa na Sheria takatifu ya Mungu, hii ilikuwa ni faida tofauti na ya kipekee – isipokuwa wewe ulikuwa ni mvunja sheria. Bwana wetu, kwa neema, pia alimsaidia, lakini ni mpaka alipodhihirisha kwamba Sheria ndiyo msawazishaji mkuu wa wanadamu, na kuwaleta wote katika hatia mbele za Mungu (Warumi 3:19).

Lakini hatimaye tunapata kuona jinsi ambavyo Bwana wetu angeweza kuonyesha neema – na kufanya hivyo kwa haki – kwa wenye dhambi, Wayahudi na Wamataifa, kwa maana katika tukio la tatu tunamwona Bwana Yesu Mwenyewe katika shida. Akiwa katika mashitaka kwa ajili ya maisha yake mbele ya wawakilishi wa sheria ya Kiebrania na Kirumi, anashtakiwa kwa kila aina ya kosa na uhalifu mbaya. Lakini katika tukio hili pia, Yeye alikataa kujibu – Hakusema chochote!

Kwanza Kayafa, Kuhani Mkuu, alimwuliza: “Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini, Yesu akanyamaza…” (Mathayo 26:62-63).

Kisha Pilato, hakimu wa Mataifa, akasema: “Je, husikii ni mambo mangapi wanayoshuhudia dhidi yako? Naye hakumjibu neno lo lote; hata liwali akastaajabu sana” (Mathayo 27:12-14).

Kwa nini Bwana wetu alikataa kujibu chochote na kujitetea? Ni kwa sababu alikuwa amekuja ulimwenguni humu ili afe kwa ajili ya dhambi za mwanadamu wote. Hata kama, wenye dhambi wote wa nyakati zote wangekuwepo hapo kumshitaki kwa dhambi zao, bado angalibaki kuwa ‘bubu’, kwa maana alisimama pale kama mwakilishi wa mwanadamu wote, ili sisi wenye dhambi tupate “kuhesabiwa haki bure kwa neema ya Mungu, kwa ukombozi ulio katika Kristo Yesu” (Warumi 3:24).

UTUKUFU UNA YEYE KRISTO YESU MILELE NA MILELE AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *