Home 2023 June 08 YEYE HUNG’AA DAIMA!

YEYE HUNG’AA DAIMA!

YEYE HUNG’AA DAIMA!

Kipindi fulani huko nyuma, nilipokuwa nikihubiri Neno la Mungu kwenye kongamano moja, nilimwona mdada moja wa umri wa kati kwenye moja ya viti vya mbele ambaye hakuwa akisikiliza lile neno nililokuwa nikihubiri.

Hata hivyo, niliweza kugundua kuwa mdada huyo alikuwa ametoka kuchumbiwa siku si nyingi na jana yake ilikuwa ndo ‘engagement’ yake! Macho yake yalikuwa yameelekezwa kwenye pete aliyokuwa nayo kwenye kidole chake cha nne cha mkono wake wa kushoto; moyo wake na akili zake, kwa hakika, vilikuwa kwa kijana aliyeweka pete kwenye kidole kile.

Akiwa na sura ya furaha usoni mwake, na huku ‘akipepesa’ kichwa chake kutoka upande mmoja hadi mwingine, alikuwa akikitazama kile kidani cha pete kutoka kila pembe. Haijalishi ni kwa jinsi gani alivyokitazama, lakini kidani kile kiliangaza kwa kung’aa, huku akiwa na shauku ya kila jirani aliyemzunguka aione ‘lulu’ hiyo; Ingawa hakuangalia wala kutathimini ubora na thamani ya kidani husika! Pete ile iling’aa kwa sababu ilizungumza naye juu yake na juu ya upendo wake kwa kijana husika, na ilikuwa ishara ya uchumba wake kwake.

Baada ya muda niliyopewa kuhudumu kupita, nami kuhitimisha ujumbe wangu wa siku hiyo, akili yangu ilirejea katika ‘kioja’ hicho. Pete iliyokuwa imechukua ufahamu, uangalifu na tafakuri za mwanadada huyu, ilinifanya nifikirie kwa upya Biblia, Kitabu kile kile tulichokuwa tukijifunza siku hiyo. Nikakichunguza Kitabu hicho kilichobarikiwa kwa uangalifu sana; nikakiangalia kutoka pembe zote na nikakiona kinang’aa! Ilinifanya nifikirie pia kuhusu Somo tukufu na kuu la Kitabu hicho, Bwana Yesu Kristo, ambaye kwake huyo sisi waamini “tumeposwa… kama bikira safi” (2 Wakorintho 11:2). Tofauti na rafiki ye yote wa duniani hii, Yeye hung’aa na haijalishi ni kwa jinsi gani mtu anavyomtazama. Chunguza maneno Yake, matendo Yake, sifa Zake za kibinafsi, kutoka pembe zote na kwa uangalifu mkubwa; Kwa vyo vyote vile utakavyomtazama, YEYE HUNG’AA DAIMA!

Utukufu Una Yeye Kristo Milele Yote AMINA

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *