Home 2023 May 12 IMANI YA IBRAHIMU

IMANI YA IBRAHIMU

IMANI YA IBRAHIMU

Imani ya Abrahamu kwa Mungu ilikuwa ni imani yenye nguvu. Mungu alipomwita aache familia yake, marafiki zake na nchi yake, alitii na “akatoka, asijue alikokwenda.” Mungu alipoahidi kuzidisha uzao wake uwe “kama nyota za mbinguni”, aliamini, ingawa hakuwa na mtoto hata! Wakati alipokuwa katika uzee wake, Mungu aliahidi kwamba bado angekuwa na mwana kupitia Sara mwenye umri wa miaka tisini sasa, Ibrahimu bado aliamini hivyo ingawa alikuwa amengoja kwa muda mrefu sana, ikionekana kana kwamba lilikuwa ni ‘ngojeo’ tupu!

Mungu alipoahidi kuwapa uzao wake nchi ile aliyokuwa amekaa, Ibrahimu aliamini, ingawa sababu zote za kuamini ‘zilibishana’ dhidi yake. Mungu alipomwomba amtoe dhabihu mwanawe, aliyezaliwa kwa kuchelewa sana maishani mwake, katika uzee wake; mwanawe ambaye ahadi zote za Mungu zilimtegemea (zilitegemezwa kwake), alitii, na kukata kauli kwamba lazima uwe ni mpango wa Mungu kumfufua kutoka kwa wafu!

Hiyo ndiyo ilikuwa imani ya Ibrahimu kwa Mungu. Mara tatu katika Warumi Sura ya Nne (4) pekee, jambo hili limesisitizwa kwa umuhimu mkubwa: Naye “aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa” (Mstari wa 18); Hakuwa “dhaifu katika imani” (Mstari 19); “Hakusita katika ahadi ya Mungu kwa kutokuamini,” bali alikuwa “mwenye nguvu katika imani” (Mstari 20).

Lakini haikuwa ‘nguvu’ ya imani ya Ibrahimu ndiyo iliyomwokoa; bali ukweli kwamba ‘lengo’ la imani yake lilikuwa ni Mungu (angalia Mwanzo 15:6):

“Akamwamini BWANA, naye akamhesabia jambo hilo kuwa haki”

Ibrahimu alikuwa ameiweka imani yake kwa Mtu sahihi. Imani yake ikawa “imara” kwa sababu tu alikuwa amemsikia na kumwamini Mungu hapo kwanza – kinyume na wengi wetu leo; walioweka imani yao katika vitu na katika matendo; zaka ikiwemo!

“Maana Maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki,” lakini “kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyemcha Mungu (asiyekuwa mtauwa), imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki” (Warumi 4:3,5).

Mwamini aliye sahili, mnyenyekevu, anayejikabidhi kwa Mungu na Neno lake, “huhesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu” (Warumi 3:24).

UTUKUFU NA UWEZA NA UKUU VINA YEYE HATA MILELE AMINA

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *