Home 2023 March 18 Kutoeleweka kwa Sheria!

Kutoeleweka kwa Sheria!

Kutoeleweka kwa Sheria!

Kuna dhana tatu potofu ambazo watu wengi huziendekeza kuhusu sheria ya Mungu na Amri zake Kumi:

Dhana ya Kwanza

Watu wengi wana maoni yenye mkanganyiko kwamba sheria ilikuwako sikuzote na kwamba lazima ilikuwa imetolewa kwa mwanadamu wa kwanza, Adamu, au kitambo kidogo baadaye. Kimsingi, Mungu alimpa Musa sheria kwa ajili ya Israeli yapata mwaka 1500 K.K., baada ya takriban miaka 2500 ya historia ya mwanadamu kupita (Yohana 1:17):

“Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.”

Kwa hiyo wanadamu waliishi duniani kwa takriban miaka 2500 bila sheria wala zile Amri Kumi.

Dhana ya Pili

Watu wengine wanadhani kwamba sheria na Amri Kumi zilitolewa kwa wanadamu wote kwa ujumla wake, wakati ukweli ni kwamba, zilitolewa kwa Israeli pekee (Kumbukumbu la Torati 5:2-3):

“Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na hukumu ninenazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuangalia kuzitenda. Bwana, Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu. Bwana hakufanya agano hili na baba zetu, bali na sisi, yaani, sisi sote tuliopo hapa, tu hai.”

Dhana ya Tatu

Watu wengine pia wanadhani kwamba sheria na Amri Kumi zilitolewa ili kutusaidia kutenda haki. Hata baadhi ya wanazuoni wetu hufundisha hivyo, ingawa Biblia inafundisha waziwazi kwamba tulipewa sheria ili kutuonyesha kwamba sisi ni watenda dhambi wenye hatia mbele za Mungu!

Ni kweli kwamba sheria, ingawa ilitolewa kwa Israeli, pia inamwonyesha Mmataifa kwamba yeye ni mwenye dhambi; mwenye hatia. Ndiyo maana Warumi 3:19 inasema:

“Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu.”

Lakini muhimu zaidi ya yote: Watu wachache wanatambua kwamba Bwana Yesu Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu ili atukomboe kutoka kwenye hukumu ya haki ya sheria. Hili linafundishwa na Mtume Paulo katika Maandiko yafuatayo:

“Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu…” (Wagalatia 3:13).

“Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye” (2 Wakorintho 5:21).

“Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu HAMWI CHINI YA SHERIA, BALI CHINI YA NEEMA” (Warumi 6:14).

UTUKUFU UNA YEYE KRISTO MILELE NA MILELE

Author: Festus Patta

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *