Home 2022 December 31 Huduma ya Mauti – Huduma ya Haki

Huduma ya Mauti – Huduma ya Haki

Huduma ya Mauti – Huduma ya Haki

“Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha. Basi, ikiwa huduma ya mauti, iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika; Je! Huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu? Kwa maana ikiwa huduma ya adhabu ina utukufu, siuze huduma ya haki ina utukufu unaozidi.” (2 Wakorintho 3:6-9)

Mtume Paulo, akilinganisha Agano Jipya na Agano la Kale, anatuonyesha kwamba “ANDIKO – Agano la Kale,” pamoja na matakwa na adhabu zake, “HUUA.” Kwa hiyo kipindi cha Sheria kinaitwa “huduma ya mauti” na “huduma ya adhabu” (2 Wakorintho 3:7,9).

Huduma ya Sheria ilianza katika mwali wa utukufu. Mlima Sinai wote ulikuwa “unatoa moshi… moshi wake ulipanda juu sana kama moshi wa tanuu.” Kulikuwa na ngurumo na umeme na tetemeko la ardhi. Kulikuwa na sauti ya tarumbeta, “kubwa sana.” Kulikuwa na wingu tukufu la Shekina ambamo Mungu Mwenyewe alionekana na “kunena maneno haya yote” (Kutoka 19:9-24).

Lakini kabla Musa hajashuka kutoka mlimani na zile mbao za mawe, watu wake tayari walikuwa wakiivunja ile amri ya kwanza kabisa, wakicheza kama wapagani ‘kumwadhimisha’ ndama wa dhahabu. Kuanzia wakati huo na kuendelea, usimamizi wa Sheria ulichukua taswira nyingine; Hukumu ilibidi itolewe na adhabu ikawekwa. Na wala hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kuepuka hukumu yake ya haki na hukumu yake ya kifo. Kile ambacho kilikuwa kimeanza katika utukufu kilisababisha huzuni, “kwa sababu sheria ndiyo hufanya ghadhabu…” (Warumi 4:15). “…kwa maana imeandikwa, amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye” (Wagalatia 3:10).

Lakini hapawezi kuwa na huzuni unaohusishwa na huduma ya Agano Jipya, amesema Mtume Paulo; kwa kuwa chini yake haki na uzima huwekwa kwa wale wote ambao watayapokea mambo yake kwa imani. Na hii ni kwa sababu madai yote ya Agano la Kale yalitimizwa kikamilifu na Kristo Yesu pale Kalvari. Hivyo huduma ya Agano Jipya inang’aa (ina utukufu unaozidi) zaidi dhidi ya huduma ya Agano la Kale kwa kila jambo.

Lakini Je! Agano Jipya halikufanywa “na nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda,” badala ya kufanywa na Kanisa la siku zetu? Ni kweli kabisa; Lakini kwa Israeli kumkataa Kristo na upofu uliowafika kwa muda, baraka za Agano Jipya sasa zinatolewa kwa neema juu ya wale wote wanaompokea Kristo. Kwa hiyo, hakuwa Mtume Petro au wale kumi na wawili, bali Mtume Paulo ambaye, pamoja na washirika wake, walifanywa kuwa “wahudumu hodari wa Agano Jipya” (2 Wakorintho 3:6).

UTUKUFU UNA YEYE MILELE NA MILELE AMINA.

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *