Home 2022 November 17 MLANGO ULIOFUNGULIWA

MLANGO ULIOFUNGULIWA

MLANGO ULIOFUNGULIWA

“Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga” (Ufunuo 3:8).

Unabii huu kuhusu kanisa la Filadelfia bila shaka unatazamia siku zijazo, lakini ni nani anayeweza kukana kwamba una somo muhimu kwa siku zetu?

Kimsingi, katika kutembea kwetu maishani, Mungu ametuwekea mbele yetu milango iliyofunguliwa ya fursa, na kwa hakika Yeye anakusudia sisi tuiingie. Njia pekee ya kuepuka kuingia kwenye mlango ulio wazi, uliowekwa mbele yetu, itakuwa ni kuikwepa fursa hiyo kimakusudi. Ole wetu, kwa jinsi tunavyojibaraguza! Kwa kuwa, mara nyingi, tunamwomba Mungu atufungulie milango wakati Yeye tayari amekwisha kuiweka wazi mbele yetu milango iliyofunguliwa na kilichobaki ni kwa sisi tu kuiingia milango hiyo…

Jipe muda wa kuchunguza rekodi ya huduma ya Mtume Paulo na ujionee jinsi yeye alivyomshukuru Mungu kwa milango iliyofunguliwa (Matendo 14:27; 1 Wakorintho 16:9), akizichangamkia fursa hizo kwa kadiri Mungu alivyoziweka wazi mbele zake; kila upande. Hakuwafunga kamba wala kuwaomba marafiki zake watumie ushawishi wao ili pengine kupitia vyeo vyao apate unafuu katika huduma yake au aweze kulipwa vizuri zaidi. Kwa uaminifu, aliuingia kila mlango ambayo Mungu aliuweka wazi mbele yake. Maombi yake yanayojulikana zaidi ya kuombea milango iliyofunguliwa yalitoka Rumi, ambapo mlango wa gereza ulikuwa umefungwa nyuma yake. Je, hili halitutii aibu; sisi ambao hatupo gerezani?

Mungu na atutie hatiani kwa kushindwa kwetu kuomba sawasawa na milango iliyofunguliwa huku tukishindwa kuingia katika milango hiyo mingi iliyofunguliwa tayari! Mungu na atusamehe pia kwa kuwa kwetu wachaguzi wa namna ya kumfanyia kazi! Na zaidi sana, atupe neema ya kutumia fursa yoyote inayojitokeza kwetu, “tukiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu” (Waefeso 5:16).

Utukufu Una Yeye Kristo, Milele na Milele; AMINA.

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *