Home 2022 November 05 UMWILISHO WA KRISTO

UMWILISHO WA KRISTO

UMWILISHO WA KRISTO

Kihistoria, ni ukweli uliothibitishwa kwamba Yesu wa Nazareti alizaliwa Bethlehemu katika siku za Mfalme Herode. Waandika Injili Mathayo na Luka wanatupa rekodi ya kuwasili kwa Bwana wetu kwa urahisi wa ajabu ambao hata mtoto mchanga anaweza kuelewa. Lakini ni Mtume wa watu wa Mataifa ndiye ambaye anaeleza umuhimu wa Umwilisho (incarnation – kufanyika mwili) kwa Kristo.

Kulingana na Fundisho la Paulo

Kristo alipoacha utukufu wake huko mbinguni, Yeye aliyekuwa Mungu, alijiondolea udhihirisho wa nje wa sifa zake. Ilikuwa ni muhimu kwamba Bwana afunike (veil) utukufu wa uungu Wake ili wanadamu wenye dhambi waweze kuwepo mbele zake.

“Ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu” (Wafilipi 2:6-7)

Kuja kwa Kristo ulimwenguni kulikuwa ni kwa njia ya asili kama kuzaliwa kwingine. Alizaliwa na mwanamke ili aweze kukamilisha kazi kuu ya ukombozi.

“Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.” (Wagalatia 4:4-5)

Bwana wetu alijinyenyekeza kwa kuingia katika umbo la mwanadamu asiye na dhambi ili apate vishawishi na majaribu yote tunayokutana nayo. Kwa hiyo, alijitwalia umbo la mtumishi ili aweze kuwahudumia wengine.

“Bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.” (Wafilipi 2:7-8)

Ndani ya chombo hiki kisafi, kisicho na dhambi, kulimwagwa dhambi na maovu yetu. Matokeo yake, Yeye alifanywa kuwa dhambi kwa ajili yetu ili haki yake ihesabiwe kwetu.

“Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.” (2 Wakorintho 5:21)

Hori la kulia ng’ombe na Msalaba vinasimama kwenye ncha tofauti za maisha ya kidunia ya Bwana wetu, lakini vimeunganishwa kwa namna ya pekee na ufunuo maalum aliopewa Paulo kwamba “Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi.”

Ingawa mapokeo mara nyingi hufunika kweli; Mungu, kwa neema yake isiyo na kikomo, atutumie kama vyombo vya kuonyesha ulimwengu uliopotea na unaokufa NJIA, ambayo ni Kristo Yesu.

Utukufu una Yeye KRISTO, Milele na Milele; AMINA.

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *