Home 2022 October 29 Msamaha Usioweza Kubatilishwa

Msamaha Usioweza Kubatilishwa

Msamaha Usioweza Kubatilishwa

Karne nyingi kabla ya Kristo, Mtunga Zaburi alisema:

“Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, Ili Wewe uogopwe” (Zaburi 130:3-4)

Inatia shaka kama Mtunga Zaburi aliuelewa msingi ambao juu yake Mungu mwenye haki, katika vizazi vyote, amekuwa akifanya hivyo – akisamehe dhambi kwa neema; Hili hata hivyo, limefunuliwa tangu wakati huo katika Nyaraka za Mtume Paulo.

Katika hizo, tunasoma: “Mungu, kwa ajili ya Kristo, amewasamehe ninyi” (Waefeso 4:32). Lakini hii ni sehemu tu ya  ile kweli, kwa kuwa Mungu huwasamehe wenye dhambi, si tu kwa sababu Kristo anatamani hili, lakini pia ni kwa sababu Kristo alilipia deni la dhambi zao na kuununua ukombozi wao kwa gharama. Hivyo Waefeso 1:7 inatangaza: “Katika [Kristo], kwa damu yake, tunao ukombozi, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.”

Na kwa sababu hiyo hiyo, Mtume Paulo aliweza kuwatangazia wasikilizaji wake katika sinagogi la Antiokia ya Pisidia:

“Basi, na ijulikane kwenu, ndugu zangu, ya kuwa kwa huyo mnahubiriwa msamaha wa dhambi; na kwa yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza kuhesabiwa haki kwa torati ya Musa” (Matendo 13:38-39).

Ni wazi kwamba msamaha huo hauwezi kamwe kufutwa au kubatilishwa, kwa kuwa unategemea malipo kamili na kamilifu ya deni letu lote la dhambi kwa “damu ya thamani ya Kristo.”

Inasikitisha kuona kwamba watu wengi hawahisi wanahitaji msamaha, kwa kuwa hawajajiona vile walivyo waovu machoni pa Mungu mtakatifu! Lakini kinyume chake, wale wanaotambua dhambi zao na wako tayari kusema pamoja na mwana mpotevu: “nimefanya dhambi,” wanaweza kupata amani na furaha kwa dhambi zao zilizosamehewa kwa imani katika Kristo ambaye alilipa adhabu ya dhambi zetu kikamilifu.

Hapa kuna msamaha ambao hauwezi kamwe kubatilishwa kwa sababu unategemea “sadaka moja [ya Kristo pale Kalvari]” ambayo kwayo Bwana wetu “amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa [yaani, waliotengwa kuwa Wake]” (Waebrania 10:14).

Utukufu una Yeye KRISTO, Milele na Milele; AMINA.

Author: Festus Patta

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *