Home 2022 August 11 Mwana wa Mtu!

Mwana wa Mtu!

Mwana wa Mtu!

Katika shuhuda nne za “Injili”, Bwana Yesu Kristo amejitaja Mwenyewe takribani mara themanini kuwa ni “Mwana wa Mtu (Adamu)”. Jina hilo limetokana na kifungu kimoja katika unabii wa Danieli ambacho kinasema kuwa “utawala, na utukufu, na ufalme” vitatolewa kwa yule atakayetokea kama “Mwana wa Mtu (Adamu)”. Ufalme huu, kimesema kifungu hicho; “hautakuwa na mwisho, na wala hautaweza kuangamizwa.”

“Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.” (Danieli 7:13-14)

Kama vile ilivyo kwa neno “Mwana wa Mungu” linavyozungumza juu ya uungu wa Bwana wetu Yesu Kristo; na neno “Mwana wa Daudi” linavyosisitiza juu ya cheo chake kama Mfalme wa Israeli; vivyo hivyo neno “Mwana wa Mtu” linamtambulisha Yeye kama mwakilishi wa wanadamu wote kwa ujumla wake.

Ni katika hali yake kama “Mwana wa Mtu” ndivyo atakavyotawala kama Mfalme wa ulimwengu; kama “Mfalme wa wafalme”; kama tulivyoona hapo juu katika unabii wa Danieli. Pia ni katika hali yake hiyo kama “Mwana wa Mtu” ndivyo atakavyohukumu mataifa yote mara tu kabla ya ufalme Wake kuanza kutawala:

“Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake” (Mathayo 25:31-32)

Vile Vile, kama Mwana wa Mtu atakuwa ni Mwamuzi katika hukumu ya mwisho katika Kiti cha Enzi, Kikubwa, Cheupe (Ufunuo 20:11-15).

“Kwa maana Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote… kwa sababu yeye ni Mwana wa Adamu” (Yohana 5:22,27).

Hakika, kama Mungu; hangeweza kuwa mwenye ‘haki zaidi’ katika kujihusishwa kwake na wanadamu. Lakini alipata ‘haki zaidi’ akiwa kama ‘Mwana wa Mtu’ ambapo; akiwa katika hali hiyo, Bwana wetu huyo alituwakilisha pale Kalvari, akilipa adhabu ya dhambi zetu ili apate kutukomboa kutoka katika hukumu ijayo. “Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja ulimwenguni… kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” (Marko 10:45). Na katika “wakati ufaao”; Mtume Paulo aliinuliwa kutangaza habari njema kwamba, Mpatanishi mkuu alikuwa amejitoa mwenyewe kuwa “FIDIA KWA WOTE” (1 Timotheo 2:6).

Utukufu una Yeye KRISTO, Milele na Milele; AMINA.

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *