Home 2022 August 10 Ufunuo wa Yesu Kristo

Ufunuo wa Yesu Kristo

Ufunuo wa Yesu Kristo

Kitabu kikuu cha mwisho cha Biblia kimeanza kwa maneno haya: “Ufunuo wa Yesu Kristo,” na kutokana na maneno hayo kimepata jina lake: “Ufunuo.” Katika kitabu hiki, Mtakatifu Yohana anaandika kwa kiasi kikubwa kuhusu kurudi kwake Kristo Yesu katika utukufu wake ili kuhukumu na kutawala.

2 Wathesalonike 1:7-8 inatuambia kwamba siku moja “wakati wa KUFUNULIWA kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu.” Hicho ndicho kitabu hiki cha Ufunuo kinahusu…! Lakini maneno haya pia yametumika katika nyaraka za Paulo, kwa kuwa katika Wagalatia 1:11-12 amesema:

“Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa UFUNUO WA YESU KRISTO”

Hakika huu si “ufunuo wa Yesu Kristo” ule ule ambao Mtakatifu Yohana aliandika habari zake. Anachokirejelea Mtume Paulo si “kufunuliwa kwake Yesu Kristo” katika utukufu ili kuhukumu, BALI “kufunuliwa kwake Yesu Kristo” katika neema huku akichelewesha hukumu; SIO ufunuo wake kwa ulimwengu katika nafsi yake, BALI ufunuo wake kwa ulimwengu kupitia kwa Paulo mkuu wa wenye dhambi, aliyeokolewa kwa neema.

Katika Mistari ya 15-16 ya Wagalatia 1, Mtume asema maneno haya: “…Mungu aliona vyema…, kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu.” Ni ufunuo ulioje wa neema kwa ulimwengu huu uliolaaniwa na Mungu wakati ule Mungu alipomwokoa Sauli, adui Wake mkuu na mkufuru! Mtume Paulo ameandika juu yake mwenyewe katika 1 Timotheo 1:13-16, ambapo anasema haya:

“Ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, LAKINI NALIPATA REHEMA kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani.  Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi. LAKINI KWA AJILI HII NALIPATA REHEMA, ILI KATIKA MIMI WA KWANZA, YESU KRISTO AUDHIHIRISHE UVUMILIVU WAKE WOTE; NIWE KIELELEZO KWA WALE WATAKAOMWAMINI BAADAYE, WAPATE UZIMA WA MILELE.”

Hii ndiyo sababu Paulo anasema: “…ilimpendeza Mungu… kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu.” Kwa kumwokoa mkuu wa wenye dhambi (kama Paulo anavyojiita katika 1 Timotheo 1:15)…

Katika hilo, Mungu ametuonyesha kwamba; yuko tayari kumwokoa mwenye dhambi yeyote, “kwa kuwa, kila atakayeliitia jina la Bwana ataokoka” (Warumi 10:13).

Utukufu una Yeye KRISTO, Milele na Milele; AMINA

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *