Home 2022 June 20 Siku ya Mambo Madogo!

Siku ya Mambo Madogo!

Siku ya Mambo Madogo!

Zerubabeli alipoweka msingi wa hekalu la pili baada ya Utekwa wa Babiloni, watu wengi wa nchi yake waliziangalia jitihada zake hizo kwa dharau, wakiamini kwamba kamwe haingekuwa na maana yoyote. Nabii Zekaria aliwajibu wakosoaji hao kwa maneno yafuatayo:

“Tena neno la Bwana likanijia, kusema, Mikono yake Zerubabeli imeiweka misingi ya nyumba hii, na mikono yake ndiyo itakayoimaliza; nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwenu. Maana ni nani aliyeidharau siku ya mambo madogo?  Kwa kuwa watafurahi, nao wataiona timazi katika mkono wa Zerubabeli; naam, hizi saba ndizo macho ya Bwana; yapiga mbio huko na huko duniani mwote.” (Zekaria 4:8-10)

Zekaria aliwakumbusha watu kwamba ingawa kazi hiyo ilionekana, machoni pao, kuwa ni ndogo, hawakupaswa kuidharau kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja na Zerubabeli!

Gideoni alipokusanya jeshi kubwa kupigana na Wamidiani, ambao walisemekana kuwa kama panzi juu ya nchi, Bwana alipunguza idadi ya majeshi ya Gideoni hadi mia tatu tu. Katika Maandiko yote kuna mada inayojirudia kwamba Mungu anapendezwa zaidi na ubora kuliko anavyopendezwa na uwingi. Kwa kadiri idadi inavyokuwa ndogo, ndivyo Anavyopokea zaidi utukufu na heshima na kuabudiwa, kama ambayo inadhihirishwa wazi katika hadithi ya ‘mia tatu’ ya Gideoni.

Tunaposonga mbele kwenye ‘korido’ hili la wakati, ingawa inaweza kuonekana kuwa HARAKATI za KUTANGAZA NEEMA YA MUNGU kuwa ni ndogo na isiyo na maana machoni pa wakosoaji wa kimadhehebu (kidini), lakini wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa kwamba wasiidharau ‘siku ya mambo madogo’. Ni kweli kuwa inaweza kuonekana kana kwamba sisi wa mlengo huu ni wadogo kwa kulinganishwa na wale wa ‘makanisa makubwa’ ya siku zetu hizi ambayo mara nyingi yanatuchukulia kuwa raia wa daraja la pili huko mbinguni. Hata hivyo, kinyume chake ndio kweli kama tutatumia kanuni hiyo hapo juu, iliyokuwepo tangu zamani. Kwa mshangao wa wale ambao kamwe HAWAUBEBI Ujumbe wa Neema ya Mungu kwa uzito unao stahili, kwenye Kiti cha Hukumu cha Kristo (Warumi 2:16), hawataamini jinsi Bwana atakavyo watambua kwa kuwavika taji ya haki (2 Timotheo 4:8) wale wote ambao kwa hiari walisimama kwa ajili ya utume na ujumbe wa Paulo kwa sifa ya utukufu Wake Yeye Kristo.

Kwa hiyo hatupaswi kamwe kuvunjika moyo kwa sababu ‘eti’ sisi ni wachache kwa hesabu/idadi, kwa maana Mungu ametuheshimu kwa kutupatia ufahamu wa Neno, ambao umegawanyika sawasawa! Lakini hii haimaanishi kwamba tujifikirie sana sisi wenyewe kuwa ni bora, zaidi sana tuone kuwa tuna wajibu tuliopewa na Mungu wa kuwaangaza watu wote wajue habari ya madaraka ya ile SIRI (Waefeso 3:9). Na ni muhimu pia kwamba tutekeleze agizo hili kwa kushika na kuisema KWELI kwa upendo (Waefeso 4:15).

Ingawa tunafurahi kwamba Kristo anahubiriwa katika duru za madhehebu, kwa sehemu kubwa, wamekengeuka kutoka kwenye kweli ya Ujumbe wa Neema ya Mungu. Tukiwa na hilo akilini mwetu, niwatie shime wote ninyi kuungana pamoja nasi katika maombi ili kuwe na amko moja kuu la mwisho kwa ndugu zetu wa ‘kimadhehebu’ kwa injili ya Paulo kabla hatujaitwa katika utukufu! Kumbuka, Mungu aweza “kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu” (Efeso 3:20).

Utukufu una Yeye KRISTO, Milele na Milele; AMINA.

Author: Festus Patta

5 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *